TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA TUHUMA ZA WAANDISHI WA HABARI
Klabu ya Waandishi wa habari ya Mkoa wa Mwanza (MPC) imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii juu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza kununuliwa na MWAUWASA ili kutoandika habari za ongezeko la bei za maji Jijini Mwanza.
MPC inawataka wadau kuzipuuza taarifa hizo kwani zina lengo la kuzichafua taasisi zetu mbili, MWAUWASA NA MPC pamoja na waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza, kupitia kwa watu wachache wasio na nia njema na taasisi hizo na wenye uelewa mdogo wa sayansi ya mahusiano na uandishi wa habari.
Ifahamike kuwa, MPC ndio iliyoingia kwenye fungate na MWAUWASA kuandaa ziara ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza kuitembelea miradi ya maji inayosimamiwa na MWAUWASA kwa lengo la kujenga ufahamu wa miradi hiyo kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza , hivyo MPC ndiyo iliyoalika waandishi mia moja(100) kwenda ziara hiyo na sio sabini kama inavyoelezwa na msambazaji wa taarifa hiyo, ambaye anaonyesha kutofahamu hata takwimu halisi.
Ndugu Waandishi wa habari ifahamike kuwa, ziara za waandishi wa habari kwenda kwenye taasisi fulani kukagua shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo siyo suala geni hapa Nchini, jambo hili linafanywa kila siku, mfano ziara za waandishi kutembelea mradi wa reli ya kisasa (SGR), waandishi kutembelea Mbuga za wanyama, waandishi kutembelea TBL na miradi mingine, msingi wa jambo hili ni kujenga mahusiano na kuwarahisishia waandishi kuzifahamu taasisi husika kwa upana.
Ikumbukwe kuwa, suala la kupanda kwa bei za maji haikuwa ajenda ya MPC kwenye kutembelea miradi ya MWAUWASA , kwani jambo hilo ni jambo la kisheria na ikumbukwe kuwa MPC haihusiki kutengeneza maudhui ya habari kwa vyombo vya habari, hivyo maamuzi ya kufuatilia ongezeko la bei za maji yalibaki kwa vyombo vya habari na sio ziara ya waandishi.
Pia MWAUWASA ilitoa nafasi ya kila Mwandishi kuuliza swali lolote alilokuwa nalo na waandishi walifanya hivyo na habari ziliandikwa juu ya sababu za kupanda kwa bei za maji, hivyo waandishi walitekeleza wajibu wao kwa kufanya uzania kwa pande zote mbili.
Ndugu waandishi, mwandishi anayesambaza taarifa hizo ameshindwa kuhoji MPC, MWAUWASA na hata Mwandishi mmoja kati ya hao sabini aliowataja, hii inayoonyesha udhaifu mkubwa wa hoja zake pamoja na kutofahamu msingi wa uandishi wa habari na sheria mama ya taaluma.(MSA Act,2016).
Mwisho MPC tunaahidi kuendelea kufanya kazi na MWAUWASA , waandishi wa habari na wadau wengine wote kwa nia ya kuchakata maendeleo ya Mkoa wa Mwanza.
Edwin Soko
Mwenyekiti- MPC
Social Plugin