Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza kupungua kwa bei ya mafuta ya taa, petroli, dizeli yanayoingizwa nchini kupitia bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga kuanzia leo.
Taarifa iliyotolewa na Ewura imesema bei ya jumla na rejareja kwa mafuta yaliyoingiziwa bandari ya Dar es Salaam imepungua huku petroli kwa Sh160 sawa na asilimia 6.9, Dizeli Sh102 sawa asilimia 4.3 na mafuta ya taa yamepungua kwa Sh81 sawa na asilimia 3.7.
Ewura imesema bei ya jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na taa yaliyoingizwa nchini kupitia bandari ya Tanga nayo imepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la Julai 3, 2019.
Taarifa hiyo imesema bei ya rejareja kwa mikoa ya Kaskazini ambayo ni pamoja na Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara nayo imeshuka.
Petroli imepungua kwa Sh134 kwa lita sawa na asilimia 5.7, dizeli Sh103 sawa na asilimia 4.6 na mafuta ya taa Sh163 sawa na asilimia 7.3.
Ewura imesema bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli yaliyoingizwa kupitia bandari ya Mtwara ambayo inahudumia mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma imepungua kwa Sh105 sawa na asilimia 4.5, Sh124 sawa na asilimia 5.3.