Takribani raia wa kigeni 600 wamekamatwa na polisi Afrika Kusini wakituhumiwa kujihusisha na uhalifu.
Operesheni hiyo maalumu dhidi ya uhalifu na watu wanaishi bila kuwa na vibali imeendeshwa na kikosi maalumu cha polisi leo Agosti 8,2019 katika jiji kuu la kiuchumi la Johannesburg.
Hata hivyo, baadhi ya raia wa nchi hiyo wamekosoa operesheni hiyo na kusema kuwa inaongeza chuki dhidi ya wageni.
Mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini yanachochewa na mdororo wa kiuchumi na ukosefu wa ajira kwa wenyeji.
Polisi wanadai kuwa "shehena kubwa" ya bidhaa bandia na silaha za moto katika majengo mbali mbali.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter kiongozi mkuu wa jimbo la Gauteng, David Makhura alisema operesheni hiyo ni sehemu ya kulifanyia usafi jimbo.
“Tunasafisha kati kati ya jiji letu. Hatutapumzika mpaka tulirejeshe jiji mikononi mwetu. Tunatuma ujumbe mkali kwa wote ambao wanahisi wanaweza kuishi kwenye majengo yetu kinyume na sheria.
“Baadhi ya raia wa kigeni ambao wanauza bidhaa bandia na kukaa kwenye majengo yetu kinyume cha sheria wamewashambulia askari wetu kwa chupa na mabomu ya petroli. Shambulio hili haliwezi kuvumilika, tutajibu kwa nguvu ya dola kulinda utawala wa sheria," aliandika Makhura katika mtandao huo.
Kwa mujibu wa polisi, katika msako huo pia shehena kubwa ya bidhaa bandia na silaha za moto zimepatikana katika majengo mbali mbali.
Social Plugin