RAIS MAGUFULI AKABIDHIWA UENYEKITI WA SADC

RAIS Dkt John Magufuli amekabidhiwa rasmi nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) huku akiitaka Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kuchukua hatua za makusudi ili kuharakisha ukuaji wa Pato la Uchumi la Taifa ndani ya Jumuiya hiyo ambalo limekuwa likishuka mwaka hadi mwaka.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo leo Jumamosi (Agosti 17, 2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ukuaji wa Pato la Taifa katika jumuiya hiyo umekuwa si wa kuridhisha, pamoja na nchi nyingi za Jumuiya hiyo kuwa na wingi wa utajiri wa raslimali.

Rais Magufuli alisema Sekretarieti ya Jumuiya hiyo haina budi kuweka mikakati na mipango madhubuti kwa Nchi wanachama ndani ya jumuiya hiyo kuhakikisha kuwa zinaweka na kuandaa mazingira bora na wezeshi yenye uwezo wa kutoa fursa za ukuaji wa uchumi ikiwemo ukuzaji wa sekta ya biashara ndani ya jumuiya hiyo.

“Mwaka 2005, 2006 na 2007 ukuaji wa Pato la Taifa ndani ya Jumuiya lilikuwa kwa asilimia 6.6 (2005), 7.3 (2006) na 8.0 (2007) lakini mara baada ya hapo ukuaji wake haukuwa wa kuridhisha ambapo mwaka 2012 ilikuwa (4.4), 2013 (4.3), 2014 (3.4), 2015 (2.2), 2016 (1.4), 2017 (3.0) na 2018 (3.1)” alisema Rais Magufuli.

Alisema ili kuweza kukuza uchumi Nchi za SADC, Viongozi wa Mataifa hayo hayana budi kuwa na viwango, sera, sheria na kanuni za pamoja zinazotoa fursa kwa nchi hizo kuwa na mfumo wa pamoja utakaowezesha jumuiya hiyo kuweza kubadilishana ujuzi, uwezo na kuuziana bidhaa na kuondoa masharti mepesi yatakayorahisha ukuaji wa uchumi.

Akifafanua zaidi, Rais Magufuli alisema pamoja na Jumuiya hiyo kujiwekea malengo kwa kila Nchi za jumuiya hiyo kukuza uchumi wake angalau kufikia kiwango cha asilimia 7 mwaka 2018 kwa kila Nchi, lakini ni nchi chache zilizofanikiwa kufikia kiwango hicho, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika katika kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinafikiwa kwa nchi zote.

Aliongeza kuwa malengo ya pamoja yanapaswa kuwekwa na Nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ndani ya jumuiya hiyo ikiwemo kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa taarifa za biashara ambazo Mataifa mengi ya Asia yamekuwa yakitumia fursa hiyo pamoja na kuimarisha na kujenga viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa vitavyowezesha kupunguza gharama za ununuzi wa bidhaa kutoka nje ya Jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema pamoja na mafanikio mbalimbali ambayo tayari yamepatikana, zipo baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiikabili jumuiya hiyo ikiwemo majanga ya binadamu, njaa na ukame ambazo zimefanya ukuaji wa uchumi katika baadhi ya nchi wanachama kuweza kuathirika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti aliyemaliza muda ambaye pia ni Rais wa Namibia Dkt. Hage Geingob alisema Jumuiya hiyo ina imani na Uongozi mpya wa Rais Dkt. John Magufuli kutokana na utendaji kazi na msisitizo alionao katika kusimamia malengo ya uanzishaji wa jumuiya hiyo katika kuleta maslahi na maendeleo ya wananchi waliopo ndani ya jumuiya hiyo.

Anaongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Uongozi wake, Jumuiya hiyo imeweza kutekeleza miradi na programu mbalimbali kupitia Mpango kazi wa miaka mitano wa Jumuiya hiyo (2015-2020) ikiwemo kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ambalo limekuwa likiongezeka siku hadi siku.

Aidha aliongeza kuwa ili kufikia Malengo mapana ya Jumuiya hiyo, Nchi wanachama hazina budi kuweka mkazo katika  kujenga ushirikiano baina ya sekta binafsi na ile ya umma kwa kutekeleza miradi na programu mbalimbali pamoja na usimamizi wa rasilimali muhimu zilizopo ndani ya jumuiya hiyo ikiwemo nishati, madini na viwanda.

Awali Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dkt. Stegomena Tax aliisifu Tanzania kutokana na kiwango kizuri cha ukuaji wa uchumi wake uliofikia asilimia 7.0 na kuwa Nchi ya mfano katika Jumuiya hiyo, hatua iliyotokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.

Aidha Dkt. Tax pia aliusifu utekelezaji wa  mradi wa kufua umeme wa maji wa Nyerere katika Maporomoko ya Mto Rufiji kwa kuwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ambayo inatarajia kumaliza changamoto ya ukosefu wa nishati ya uhakika katika Nchi za SADC.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post