John Seka Afisa mtendaji mkuu wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani nchini (RSA) akizungumza na mabalozi katika mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika Jijini Mwanza.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Marlin Komba ,akisisitiza jambo katika mkutano mkuu wa mwaka wa mabalozi wa usalama barabarani uliofanyika Jijini Mwanza.
Mabalozi wa usalama barabarani nchini wakiwa katika mkutano mkuu wa Mwaka uliofanyika Jijini Mwanza
Moja ya timu wapenzi na marafiki wa Simba Sports Club wakiwa uwanjani kwa ajili ya mchezo wa kirafiki katika Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza
Moja ya timu wapenzi na marafiki wa Yanga sports Club wakiwa uwanjani kwa ajili ya mchezo wa kirafiki katika Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Baadhi ya mabalozi wa Usalama barabarani wakiwa katika picha ya pamoja
Mabalozi wa usalama barabarani wakionekana katika picha ya pamoja
Na .Vero Ignatus ,Mwanza
Zaidi ya mabalozi 125 kutoka Taasisi ya Mabalozi wa Usalama barabarani( RSA ) wamekutana Jijini Mwanza,lengo kuu likiwa ni kutoa elimu na kuwajengea wananchi uwezo wa kuwa sehemu ya mabadiliko ya usalama barabarani ikiwa ni namna ya kusaidia
kupunguza ajali ,kwani kila raia wa Tanzania anawajibu wa kuwa sehemu ya mabadiliko ya usalama barabarani.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Agosti 30,2019 jijini Mwanza,Afisa mtendaji Mkuu wa Taasisi ya mabalozi wa usalama barabarani nchini, John Seka alisema kwa kushirikiana na jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza kikisimamiwa na RTO,Tanroad ,Jeshi la zimamoto, walifanya zoezi za kurudishia alama za barabarani zile zilizopauka ,na kuchora mpya sehemu zinazohitajika.
Seka alisema kuwa kazi zao kubwa kama RSA ni kukemea, kuelimisha ,kutoa taarifa pale dereva anapokwenda kinyume na taratibu na sheria za usalama barabarani ili kuhakikisha kuwa ajali zinapungua kama siyo kwisha kabisa
“Sisi tunafanya kazi zetu kama polisi jamii,macho yetu tunayaelekeza kwa kutambua kuwa jeshi la polisi peke yao hawawezi kwani askari ni wachache na vitendea kazi ni vichache je! sisi kama wananchi hatuna wajibu wa kupunguza?", alihoji Seka.
Mkurugenzi wa tafiti za kisheria kutoka RSA,Augustus Fungo alisema pamoja na kuwa balozi lazima wazingatie sheria za usalama barabarani pia lazima wafuate sheria kama utaratibu unavyoagiza
Alisema hadi sasa RSA wanatekeleza mradi wa Maboresho
ya sheria ya usalama barabarani,wenye lengo la kushawishi serikali na bunge kubadili sheria ya usalama barabarani ya
mwaka 1973 ili ikidhi mahitaji ya wakati huu kwasababu ina mapungufu katika maeneo mbalimbali.
"Mfano wa mapungufu hayo ni pamoja na sheria ya sasa kutomlazimisha abiria kuvaa kofia ngumu,kufunga mkanda,kutokulazimu magari madogo kuwa na vizuizi vya watoto wakiwa ndani ya gari (child restraint) Sheria pia hailazimishi magari yote kusimama kabla ya kuvuka kivuko cha reli isipokuwa magari ya abiria na mizigo",alisema Fungo.
Alisema hadi sasa RSA imefanikiwa kufungua klabu za usalama barabarani kwa wanafunzi katika shule 22,ambapo 10 kutoka mkoa wa Kilimanjaro,12 mkoa wa Pwani, amesema matazamio ya baadaye ni kupanua wigo wa shule zinazopata elimu ya usalama barabarani nchini Tanzania.
“Kwa kuwa tunaamini watoto wakifundishwa tangu wakiwa wadogo ni rahisi wao kuelewa zaidi kwao kutii sheria na
kujiepusha na ajali”,alisema Fungo.
Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba alimtaka kila balozi kutimiza wajibu wake kwa
kuzingatia maadili,bila kuwa na ushabiki wowote,pasipo kuwatetea wavunja sheria za usalama barabarani,badala yake watumie ubalozi wao kwenye kuelimika na kupata maarifa.
Aliwataka kwenda kuwa mabalozi kwa watu wengine ili kufanya maamuzi sahihi kuzingatia sheria na usalama barabarani ,na kuepuka lugha za matusi kwani ni kosa la jinai,huku akiwaonya baadhi ya mabalozi kutokutumia nembo ya RSA kukashfu watu
wengine.
Mkutano huo uliambatana na michezo mbalimbali ukiwemo mchezo wa mpira wa miguu,kuvuta kamba kufukuza kuku na mbio za magunia ,ambapo michezo yote ilifanyika katika uwanja wa mpira wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Kauli mbiu ya Mkutano wa mabalozi wa usalama barabarani ni 'Uchumi wa Viwanda unahitaji kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya Usalama Barabarani,ili kulinda rasilimali watu dhidi ya ajali'.
Social Plugin