Mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini Mhe. Wilfred Muganyizi Rwakatare (Chadema) amepongeza Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti kwa kasi nzuri ya utendaji kazi inayochangia mkoa huo kuwa na maendeleo makubwa kwa muda mfupi huku akiwataka watendaji wa taasisi mbalimbali mkoani Kagera kutambua majukumu yao.
Rwakatare ametoa kauli hiyo katika mkutano wa wafanya biashara wa Tanzania (KAGERA ) na wafanya biashara kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Burundi,Kenya Rwanda na Uganda uliofanyika katika ukumbi wa Elct uliopo Manispaa ya Bukoba wakati wa wiki ya uwekezaji Kagera.
Mbunge huyo ametaja kushangazwa na kasi ya utendaji kazi wa mkuu huyo wa mkoa kitendo ambacho kimesababisha mkoa huo kusonga mbele kwa haraka.
Aidha alimuomba mkuu huyo kuwa anakutana na wafanyabiashara wadogo na wakubwa mara kwa mara ili kujua changamoto zinazowakabili kupitia majadiliano na kuzifanyia kazi ili Kagera ikue kiuchumi
Rwakatare pia alikemea tabia ya baadhi ya wafanyakazi wanaofanya kazi kwa mazoea kwani wanachangia kurudisha nyuma maendeleo.
Hata hiyo aliwataka viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa kujenga umoja na ushirikiano ili mkoa wa Kagera usonge mbele.
Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog Bukoba
Social Plugin