Jeshi la Polisi nchini limezuia safari za saa 24 za mabasi kwa baadhi ya mikoa kwa sababu ya kiusalama na kuwataka wamiliki wa mabasi hayo kuzingatia maagizo yaliyotolewa ili kulinda usalama wa wananchi.
Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 2 na Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo, Liberatus Sabas ambapo amesema licha ya kuruhusu mabasi yote nchini kutembea usiku bila kulala sehemu yoyote, Jeshi la polisi limebaini kuna baadhi ya maeneo zoezi hilo limebidi lisubiri kidogo ili wajipange kwa ajili ya usalama na watakapojiridhisha safari hizo zitaendelea kama kawaida.
Sabas amesema mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi hayataruhusiwa kutembea saa 24 kutokana na sababu za kiusalama.
Kamishna Sabas amesema zuio hilo litahusu pia mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea wilaya mbalimbali za mkoani Tabora ambayo yatalazimika kusimama Tabora Mjini na baadaye kuendelea na safari wilayani.
Amesema mabasi yanayotoka mikoa ya Kagera, Katavi, Kigoma kwenda Dar es Salaam yataruhusiwa kutembea saa 24 kama kawaida kutokana na eneo la Morogoro na Dar es Salaam kuwa salama wakati wote.
"Mabasi haya yalikuwa yakitoka kwenye mikoa hiyo yalikuwa yanalala Morogoro, lakini kutokana na hali nzuri ya kiusalama yataendelea na safari hadi Dar es Salaam," amesema Kamishna Sabas.
Amesema mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea katika mikoa hiyo yatalazimika kulala wilayani Kahama kisha kuendelea na safari.
Social Plugin