Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ameagiza watendaji wa idara ya udhibiti ubora wa shule kusimamia kwa makini miradi ya ujenzi wa ofisi za Uthibiti ubora wa shule pamoja na fedha zinazotumwa kwa ajili ya ujenzi huo katika Halmashauri za wilaya mbalimbali nchini.
Naibu Waziri Ole Nasha amesema hayo mkoani Geita wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya Elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayehujumu ama kutumia vibaya fedha hizo zilizotolewa na wizara kwa ajili ya kujenga ofisi hizo.
Amesema miradi ya ujenzi wa ofisi hizo ni muhimu sana kwa wizara kwani ili kuwa na maendeleo katika sekta ya elimu lazima kuwa na wadhibiti ubora wa shule mahiri, wenye uwezo wa kukagua shule na wenye vitendea kazi vya kuwezesha kufanya kazi katika mazingira sahihi.
“Kama tunataka kuwa na maendeleo katika sekta ya Elimu lazima kuwe na usimamizi thabiti na ndio maana tumechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tumeboresha idara ya uthibiti ubora kwa kuhuisha mfumo kutoka kuwa ukaguzi na kuwa uthibiti kwa maana kwamba unashirikisha kila mtu katika hatua zote,” amesema Ole Nasha.
Ole Nasha amesisitiza kuwa haiwezekani kufanya kazi ya uthibiti ubora wa shule kama hakuna ofisi, vitendea kazi ikiwemo magari na ndio maana kila Afisa Elimu wa Kata kwa nchini nzima alipewa pikipiki ya kumwezesha kufanya kazi. Serikali pia ilitoa magari 45 kwa wilaya mbalimbali na sasa halmashauri zipatazo 100 zinajengewa ofisi za uthibiti ubora.
Naibu Waziri Ole Nasha amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi hizo, Wizara itapeleka vifaa vyote muhimu kwenye ofisi hizo ili kurahisisha kuchakata taarifa zote za elimu kutoka maeneo yote ya nchini kwa lengo la kurahisha huduma za kielimu.
Aidha, Waziri Ole Nasha amesema ameridhishwa na usimamizi na matumizi ya fedha za ujenzi wa ofisi za uthibiti ubora Kanda ya Ziwa ambayo inajumuisha Mikoa ya Geita, Mwanza na Mara ambayo kwa ujumla inajengewa ofisi 15 zenye thamani zaidi ya bilioni 2.28.
Katika ziara hiyo Waziri Ole Nasha amekagua majengo ya uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri ya mji wa Geita. Ole Nasha pia amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni mawili na vyoo katika shule ya sekondari Mwatulole ambayo inatarajiwa kuanzisha kidato cha tano hivi karibuni.
Shule nyingine aliyotembelea ni shule ya sekondari ya Wasichana Nyankumbu ambapo ametembelea chumba cha kompyuta na ameahidi kupeleka kompyuta 50 shuleni hapo ili kuongeza ari ya kujifunza.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka alimweleza Naibu Waziri kuwa ameshirikiana na watendaji wengine kufanikisha ujenzi ambao uko kwenye hatua ya ukamilishaji na kuahidi kuwa ataendelea kusimamia ili jengo hilo likamilike kwa wakati
Social Plugin