Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali inaangalia njia mbadala ya ununuzi wa magari yake kwa kwenda moja kwa moja kiwandani bila kupitia kwa mawakala kutokana na gharama kuwa juu na hazitabiriki.
Hayo yalibainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kubaini changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 kwa taasisi hiyo.
Dkt. Kazungu alisema kuwa, ununuzi wa magari ya Serikali unatumia gharama kubwa kutokana na kuwatumia Mawakala wa Ununuzi ambao bei zao ni za juu na zinabadilika mara kwa mara, hivyo kuna haja ya kwenda moja kwa moja kiwandani ili kuokoa fedha za walipakodi zinazopotea.
Aidha Serikali inaangalia namna itakavyo boresha miundombinu ya GPSA hasa kwa kuwekeza katika Visima vya mafuta ili kuwa na mafuta ya kutosha hivyo kusaidia kuongeza ufanisi katika kuhudumia magari ya Serikali.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa GPSA, Dkt. Geraldine Rasheli, alimshukuru Dkt. Kazungu, kwa kutembelea taasisi yake na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa ili kupunguza malalamiko katika utoaji huduma na kuongeza tija kwa Taifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Kazungu, anaendelea na ziara ya kikazi katika taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, kuangalia changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na njia za kuzitatua kwa bajeti ya mwaka 2019/20.
Social Plugin