Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali imedhamiria kutumia zaidi wataalam wake wa ndani katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kazi walizopewa.
Amesema maamuzi hayo yamekuja baada ya wataalam hao kufanya kazi nzuri, zinazochukua muda mfupi kukamilika, zenye viwango na kwa gharama nafuu ukilinganisha na wakandarasi ambao kazi zao zimekuwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha juhudi za Serikali kumaliza tatizo la maji.
Naibu Waziri Aweso amesema kwa muda mrefu Serikali imekuwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini kutokana na ubabaishaji wa wakandarasi licha ya kutumia fedha nyingi kwa dhumuni la kufikisha huduma ya maji kwa kila mwananchi.
‘‘Tumekuwa na utaratibu wa kuwapa kazi Wataalam Washauri ya usimamizi wa ujenzi wa miradi kwa gharama kubwa, lakini wamekuwa wakishirikiana na wakandarasi kuihujumu Serikali kwa kutotimiza wajibu wao na kuingizia Serikali hasara kubwa’’, Naibu Waziri Aweso amefafanua.
‘‘Baada ya kugundua tatizo hilo tukaamua kutumia wataalam wa ndani waliopo kwenye mamlaka za maji, wahandisi wa mikoa na wilaya kwenye miradi mingi iliyokuwa imekwama au ujenzi wa miradi mipya kwa gharama ndogo na kupata mafanikio makubwa, Aweso ameeleza.
Akieleza kuwa baadhi miradi mingi iliyosimamiwa au kutekelezwa na wataalam wa ndani katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Kigoma, Mbeya na Kanda ya Ziwa imekuwa na mafanikio makubwa, jambo ambalo limeifanya Serikali kudhamiria kutumia zaidi wataalam hao na kuachana na wakandarasi wababaishaji kwa lengo la kupata matokeo mazuri.
Awali, Naibu Waziri Aweso alichukua hatua ya kumkamata Mkandarasi wa Kampuni ya Mbeso Construction Ltd kwa sababu ya kusuasua kwa ujenzi wa miradi ya maji ya Munge na Tella Mande iiliyopo katika Wilaya za Siha na Moshi, mkoani Kilimanjaro bila sababu za msingi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Aweso kukagua Mradi wa Maji wa Munge, wilayani Siha na kutoridhiswa na kasi ya mkandarasi na muda wa utekelezaji wake ukiwa umebaki mwezi mmoja na kazi ikiwa ni asilimia 25 hali akiwa hana madai yoyote ya fedha kwa Serikali.