Na WAJMW-Brazzaville
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na Waziri wa Afya wa Marekani Amiral Brett Giroir na kufanya mazungumzo na kuona namna gani nchi hizo mbili zinavyoweza kushirikiana katika kupambana na ugonjwa wa Sickle Cell (Seli Mundu) hasa kwa watoto wachanga na wale walio chini ya miaka mitano.
Waziri Ummy amemueleza Waziri huyo kuwa watoto wapatao 11,000 wanazaliwa na ugonjwa huo Tanzania na wengi hupoteza maisha kwa sababu ya kuchelewa kufanyiwa vipimo na kugundulika mapema.
Waziri Ummy amemueleza kuwa muelekeo wa nchi sasa ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anayezaliwa anapimwa Sickle Cell na watakaogundulika matibabu yaanze mapema ili kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Mawaziri hao wamekubaliana kwa pamoja kushirikiana katika kudhibiti vifo vinavyoweza kutokea kwa sababu ya ugonjwa huo huku Waziri Amiral akiahidi kuimarisha upatikanaji wa vipimo, pamoja na matibabu kwa watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo kuanzia ngazi ya zahanati na vituo vyote vya kutoa huduma za afya ya msingi nchini.
“Ni muhimu huduma hizi zikatolewa katika ngazi ya afya ya msingi mpaka taifa ili kuwapa huduma stahiki wananchi, hii ikiwa ni utekelezaji wa afya kwa wote. Suala la upimaji wa Seli Mundu, elimu kwa jamii na pia suala la matibabu katika ngazi zote za utoaji huduma ni muhimu vikapewa kipaumbele”. Aliongeza Waziri Ummy.
Hivi sasa huduma hii hapa nchini inapatikana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufa za Mikoa za Amana na Temeke pekee kwa nchi nzima.
Kwa upande wake Waziri Brett amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kujenga viwanda vya dawa nchini ikiwa ni pamoja na za Sickle Cell. Pia ameahidi kutembelea Tanzania kuona na kujadiliana zaidi namna nchi hizi mbili zitavyoshirikiana katika kushughulikia ugonjwa huu nchini.
Mawaziri hao wanahudhuria mkutano wa 69 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaojumuisha Mawaziri wa Afya toka nchi mbalimbali za Afrika unaoendelea jijini Brazzaville nchini Jamhuri ya Kongo.
Social Plugin