Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIMBA SC YAAMBULIA SARE 1-1 NYUMBANI NA UD SONGO


MABINGWA wa Tanzania, Simba SC wametolewa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na UD Songo ya Msumbiji katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.


Matokeo hayo yanamaanisha UD Songo inasonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini, kufuatia kulazimishwa sare ya 0-0 mjini Beira wiki mbili zilizopita.

Na sasa watamenyana na FC Platinum ya Zimbabwe iliyowatoa jirani zao, Big Bullets ya Malawi kwa mabao 3-2 ushindi wa ugenini jana kufuatia sare ya 0-0 nyumbani wiki mbili zilizopita. 

Uwanja wa Taifa leo UD Songo waliwatangulia Simba SC kwa bao la dakika ya 14 lililofungwa na Luis Miquissone kwa shuti la mpira wa adhabu, akiutmia mwanya wa mshambuliaji Mnyarwanda Meddie Kagere kutoka kwenye kupenyeza mpira na kufunga kiulaini.

Baada ya kupambana kwa muda mrefu, hatimaye Simba SC ilifanikiwa kusawazisha hilo dakika ya 87 kwa mkwaju wa penalti wa Nahodha wa leo, Erasto Edward Nyoni kufuatia Miraj Athumani ‘Madenge’ kuchezewa rafu kwenye boksi.

Simba SC ilijitahidi kutumia dakika zilizosalia – pamoja na tatu za kufidia kusaka bao la pili, lakini wachezaji wa UD Songo walikuwa makini mno kujilinda na kufanikiwa kusonga mbele.

Simba SC inaungana na KMKM ya Zanzibar kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-0, ikichapwa 2-0 kila upande nyumbani na ugenini na Primiero de Agosto ya Angola.

Yanga pekee imesonga mbele katika Ligi ya Mabingwa baada ya ushindi wa jumla wa 2-1, ikishinda 1-0 ugenini jana dhidi ya Township Rollers kufuatia sare ya 1-1 nyumbani wiki mbili zilizopita na itamenyana na Zesco United ya Zambia iliyoitoa Green Mamba ya Eswatini kwa jumla ya mabao 5-0, ikishinda 2-0 ugenini na 3-0 nyumbani.

Katika Kombe la Shirikisho Azam FC imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia ikifungwa 1-0 ugenini na kushinda 3-1 nyumbani na itamenyana na itamenyana na Triangle United ya Zimbabwe iliyoitoa Rukinzo ya Burundi kwa mabao 5-0, ushindi wa nyumbani kabla ya sare ya 0-0 ugenini.

Malindi SC ya Zanzibar pia imefanikiwa kwenda Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mogadishu City na sasa watamenyana na Al-Masry ya Misri katika hatua inayofuata.
Timju zote za Tanzania zilizosonga mbele zitaanzia nyumbani tena kati ya Septemba 13 na 15, kabla ya kusafiri kuwafuata waponzani wao Zambia, Zimbabwe na Misri kwa mchezo wa marudiano kati ya Septemba 27 na 29.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Gardiel Michael/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk77, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Deo Kanda, Jonas Mkude, Sharaf Eldin Shiboub/Miraj Athumani ‘Madenge’dk62, Clatous Chama, Francis Kahata/Hassan Dilunga dk24 na Meddie Kagere.

UD Songo: Leonel Mario, Frank Banda/Cremildo Khantumbo dk57, Amade Momade/Micupel Tembe dk83, John Banda, Infren Matola, Luis Miquissone, Pachoio King, Hermenegildo Mutambe, Pascoal Amorim, Stelio Ernesto/Mario Sebastian dk69 na Antonio Chirinda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com