TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UWEPO WA MALIKALE MADINI NA VITU VYA THAMANI

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inapenda kuufahamisha umma na wadau wote wa sekta ya madini nchini kuwa kwa kipindi kirefu kumekuwepo na mitazamo mbalimbali juu ya uwepo wa malikale madini na vitu vya thamani  vilivyoachwa na wakoloni.


Kutokana na mitazamo hiyo, GST imekuwa ikifanya tafiti katika maeneo mbalimbali ili kubaini viashiria vya uwepo wa malikale madini ambazo zinasadikiwa kuwa zilifukiwa chini ya ardhi na wakoloni hasa wa Kijerumani baada ya vita ya pili ya dunia1939-1945. 

Baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa utafiti ni:

•    Tarehe 16/1/2019 mpaka 21/1/2019, GST ilifanya utafiti katika  Kitongoji cha Ngarawani, kata ya Uwanja wa Ndege,Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara , juu ya kubaini viashiria vya uwepo wa malikale na vitu vya thamani vinavyosadikiwa kufichwa au kutunzwa ardhini.
.
•    Tarehe 27/2/2018 mpaka 7/3/2018, GST ilifanya utafiti katika Kijiji cha Vumba Kata ya Lugulu,wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na Kitongoji cha Kakindu, kata ya Pongwe mtaa wa Pongwe Kusini Manispaa ya Tanga juu ya kubaini viashiria  vya uwepo wa malikale madini na vitu vya thamani  vinavyosadikiwa kufichwa au kutunzwa ardhini.

•    Tarehe 15/1/2016 GST ilifanya utafiti juu ya kusadikiwa kupotea kwa jiwe la thamani aina ya Almasi linalosadikiwa kufichwa katika shimo la Muhanga, katika kitongoji cha Manawa, kata ya Nkalalo, wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.

Tafiti zote hizi zilitumia njia ya Jiolojia na Jiofizikia ambazo kisayansi zinaonesha mabadiliko ya asili ya sumaku ya dunia (magnetic survey), lengo la kutumia njia hizi ni kujua kama kweli malikale hizo zitakuwa zimehifadhiwa chini ya ardhi. Kwa kutumia njia tajwa hapo juu, kisayansi viashiria vya malikale vingekuwa katika maumbo madogo kulingana na vilipohifadhiwa kama vile umbo la mraba, mstatiri kuwakilisha sanduku au umbo la mviringo kuwakilisha pipa au chungu. Hata hivyo mahojiano ya kina yalifanyika ili kujua chanzo cha habari za malikale katika eneo hilo.

Matokeo ya tafiti  hizi yameonesha wazi kuwa maeneo yote yaliyofanyiwa utafiti, hayaoneshi viashiria vyovyote vya uwepo wa malikale madini wala vitu vya thamani. Sambamba na tafiti hizo mahojiano ya kina  yaliyofanyika miongoni mwa baadhi ya wanafamilia na jamii zinazozunguka maeneo husika  ili kujua sababu za  hisia za kuwepo malikale ambapo, majibu yote yalionesha ni usadikishwaji wa uwepo wa malikale katika maeneo hayo kwa kupewa hadithi (narrated stories) ambazo ndani yake zimejaa imani mbalimbali ikiwa ni pamoja na matambiko / ushirikina juu ya malikale.

Pamoja na imani hizo GST, itaendelea kufanya tafiti zake za Jiosayansi na kutoa elimu kwa jamii juu ya njia sahihi za  utafutaji madini katika makundi mbalimbali kwa lengo la  kuepusha jamii kupoteza muda, rasilimali fedha, mtaji na kuepusha kutokea kwa matukio yanayoendana na imani za kishirikina kama vile mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, watu wenye vipara na wanawake wenye ndevu.

IMETOLEWA NA;
TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA

23/08/ 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post