Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAARIFA YA MFUMUKO WA BEI KWA MWEZI JULAI 2019


Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini ambapo pamoja na mambo mengine mfumuko wa bei ya mwezi Julai 2019, umebakia kuwa asilimia 3.7 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2019.


Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Ijumaa (Agosti 9, 2019) Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Minja alisema kiwango hichi kubakia kuwa sawa kwa kiwango hicho kumechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi za vyakula na bidhaa zisizo za chakula kwa kipindi kilichoisha Julai 2019.

Aidha Minja alisema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai 2019 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 2.9 kutoka asilimia 2.3 ilivyokuwa kwa mwezi Juni 2019.

“Baadhi ya bidhaa zilizoongezeka bei kwa mwezi Julai zikilinganishwa na Julai 2018 ni pamoja na unga wa mahindi (6.0%), unga wa mhogo (4.0%), mafuta ya kupikia (8.9%), na mbogamboga (4.6%) ambapo kwa uoande wa bidhaa zisizokuwa za vyakula ni pamoja na vifaa vya kieletroniki, majiko ya gesi pamoja na vifaa pamoja na bidhaa za huduma”.

Akizungumzia hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki, taarifa inaonyesha kuwa Nchi ya Kenya ilikuwa na Kiwango cha juu cha mfumuko wa bei kwa mwezi Julai 2019, ambapo kiwango chake kilifikia asilimia 6.27 ikilinganishwa na asilimia 5.70 kwa mwaka ulioishia Juni 2019.

Akifafanaua zaidi Minja alisema taarifa ya mfumuko wa bei katika Nchi ya Uganda katika mwaka ulioishia Julai 2019, taarifa zinaonyesha kuwa Nchi hiyo ilikuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa mdogo bei kilichofikia asilimia 2.6 kutoka asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Juni, 2019.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com