Na.Catherine Sungura,WAMJW-DSM
Serikali kupitia wizara ya afya imepiga hatua katika kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchi.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa wa Wizara hiyo, Dk. Elius Kwesi wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mapitio ya shuguli wa mpango wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele na mpango kazi wa mwaka.
Dkt.Kwesi alisema mkutano huo ni muhimu kwani watajadiliana na wadau hao kuona namna watakavyoshirikiana na Wizara hiyo kwa upande wa rasilimali fedha.
“Tuna pengo la rasilimali mbalimbali na tumewaita hapa Wadau kujadiliana nao Mpango kazi wetu na kuangalia namna gani watatusaidia kuziba pengo na kutakavyosaidiana kutekeleza,” alisema Dkt.Kwesi
Alisema tangu utekelezaji wa Mpango huo ulipoanza nchini umefanikiwa kupunguza magonjwa hayo kwa kiwango cha asilimia 80.
Awali Mkurugenzi wa huduma za Kinga wizarani hapo Dkt.Leonard Subi alisema magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yasipodhibitiwa yatapelekea watu wengi kuugua siku zijazo kwani yana athari kubwa na kusababisha upofu na ulemavu kwa jamii.
“mfano ugonjwa wa kichocho kwa watoto huathiri ukuaji na wengine wanaweza kupata saratani katika maisha yao”.Alisema Dkt.Subi
Alisema wizara kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanya jitihada kubwa na hivyo kufanikiwa kudhibiti magonjwa hayo kwa kiwango kikubwa
“Wilaya ambazo zilikua zimeathirika sana na matende na mabusha miaka kumi iliyopita zilikua takribani 120 lakini hivi sasa zimebaki wilaya 24 ambazo bado tunaendelea na ugawaji kingatiba na trakoma kulikuwa na wilaya 71 na sasa zimebaki wilaya sita tu”.
Naye Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele(NTD) Dkt.Upendo Mwingira amesema kwa upande wa kichocho na minyoo ya tumbo bado inahitajika kuendelea kuwakinga watoto na baadhi ya wilaya wanaendelea kugawa kingatiba za matende na mabusha pamoja na usubi.
Social Plugin