NA SALVATORY NTANDU
Chama cha Mapinduzi wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga (CCM) kimemwagiza Meneja wa Wakala wa barabara za mijini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Job Mutagwaba kuhakikisha anasimamia kikamilifu barabara za mitaa katika kata za Majengo ambazo zimejengwa na wananchi.
Agizo hilo limetolewa na katibu wa (CCM) Emmanuel Mbamange wakati akikabidhi fedha tasilimu shilingi laki saba kwa kamati ya ukarabati wa barabara hizo ambazo zimetolewa na mbunge wa jimbo la Kahama mjini Jumanne Kishimba.
Amesema atahakikisha (TARURA) inazikarabati barabara hizo ambazo zimekarabatiwa kwa nguvu za wananchi ili kuwezesha kupitika kwa urahisi ambapo mpaka sasa jumla ya kilomita 15 zimeshakamilika kujengwa na fedha iliyotumika ni ya kuchangishana wao kwa wao.
Amefafanua kuwa endapo barabara hizo zisipotunzwa ikiwa ni pamoja na kuwekewa changarawe na mitaro hazitaweza kudumu na nguvu kazi ya wananchi itakuwa haina tija yeyote hivyo CCM itahakikisha inawaunga mkono wananchi hao ambao wameonesha nia ya kukarabari barabara katika maeneo yao.
Naye Steveni Lutego mjumbe wa kamati ya ujenzi wa barabara hizo ameomba kuungwa mkono na serikali katika kujenga mitaro katika maeneo korofi ambayo kipindi cha mvua maji huwaathiri ili kuzuia kutokea kwa maafa yatokanayo na uharibifu wa miundo mbinu ya barabara pamoja wa ujenzi holela wa makazi katika njia za maji.
Jumla ya shilingi milioni nne laki 3 na elfu themanini zimetumika katika kukarabati barabara hizo za mitaa ambazo zinaurefu wa kilomita 15.
Social Plugin