Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : TUME YA UCHAGUZI YAKUTANA NA WADAU SHINYANGA..UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA KUFANYIKA AGOSTI 26 HADI SEPT 1,2019

Kamishina wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa nchini Tanzania,Mhe. Balozi Omari Ramadhani Mapuri amefungua mkutano wa wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Mkutano huo umefanyika leo Alhamis Agosti 15,2019 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na mkurugenzi wa uchaguzi,mratibu wa uandikishaji wa mkoa,viongozi wa dini,vyama vya siasa,wawakilishi wa watu wenye ulemavu,vijana,wanawake,asasi za kiraia,watendaji wa tume na waandishi wa habari.

Balozi Mapuri alisema lengo la mkutano huo ni kupeana taarifa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ulioanza kwa awamu ya kwanza tarehe 18 Julai,2019 katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Alisema uzinduzi rasmi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura ulifanyika Mjini Moshi Julai 18 ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na kwamba katika mkoa wa Shinyanga uboreshaji wa daftari la wapiga kura utafanyika Agosti 26 hadi Septemba 1,2019.

"Lengo la kukutana nanyi leo ni kuwafahamisha kuwa tume imekamilisha maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,ikiwemo uhakiki wa vituo vya kujiandikisha,uandikishaji wa majaribio,maandalizi ya vifaa vya uboreshaji wa daftari,maandalizi ya vifaa vya uboreshaji na mkakati wa elimu ya mpiga kura naamini mafanikio ya zoezi hili yanategemea nyinyi wadau",alieleza.

"Tume inatarajia kuanza uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa awamu ya nne katika mikoa ya Mwanza (halmashauri ya wilaya Kwimba),mkoa wa Shinyanga na mkoani Geita (Halmashauri ya Mji wa Geita,Nyang'wale,Bukombe na Mbogwe) kuanzia Agosti 26 hadi Septemba 1,2019",aliongeza.

Alifafanua kuwa uboreshaji wa daftari la wapiga kura unafanyika kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki ya Biometriki (BVR) ambayo huchukua taarifa za kibaiolojia za mtu na kuzihifadhi katika Kanzidata(Database) kwa ajili ya utambuzi.

"Uboreshaji wa daftari la wapiga kura wa safari hii hautahusisha wapiga kura walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2015 ambao kadi zao hazihitaji marekebisho yoyote ya taarifa.Uboreshaji huu utawahusu wapiga kura wapya ambao wametimiza umri wa miaka 18 na wale ambao watatimiza umri wa miaka 18 siku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.",alisema Balozi Mapuri.

Alisema uboreshaji huo pia utahusisha watu ambao wamehama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine ya uchaguzi na wale ambao kadi zao zimeharibika au kupotea na wale ambao wanatakiwa kufutwa kwenye daftari baada ya kupoteza sifa wakiwemo waliofariki dunia.

Kwa upande wake, Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Frank Mhando aliwataka watu wenye sifa ya kujiandikisha wajitokeze kwa wingi ili waandikishwe na wanaohitaji kuboresha taarifa zao wakati ndiyo huu.

Alisema kila chama cha siasa kina wajibu wa kuweka wakala kwenye kituo cha uandikishaji daftari la wapiga kura huku akikisisitiza kuwa wakala hapaswi kuingilia majukumu ya tume ya uchaguzi na kwamba yeyote atakayeleta masuala ya siasa kwenye vituo atachukulia hatua.

Aliwataka wanasiasa kuepuka kufanya siasa kwenye vituo bali majukumu yao yawe ni kuwatambua wenye sifa ya kujiandikisha wapate sifa ya kupiga kura wakati wa uchaguzi.

"Hakuna uchaguzi bila wapiga kura,hakuna kupiga kura bila kujiandikisha,niwaombe wanasiasa mhamasishe watu wajitokeze kwenda kujiandikisha ili wawe na sifa ya kupiga kura",aliongeza.

ANGALIA PICHA
Kamishina wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa nchini Tanzania,Mhe. Balozi Omari Ramadhani Mapuri akifungua mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura leo katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kamishina wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa nchini Tanzania,Mhe. Balozi Omari Ramadhani Mapuri akifungua mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga.
Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Frank Mhando mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga.
Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Frank Mhando akiwataka watu wenye sifa ya kujiandikisha wajitokeze kwa wingi ili waandikishwe kwenye daftari la wapiga kura.
Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini,Charles Shigino akiiomba Tume ya uchaguzi kuruhusu mikutano ya hadhara ili wanasiasa waelimishe/wahamasishe wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Katibu wa Chama cha ACT-Wazalendo mkoa wa Shinyanga Sebastian Tafuta akichangia hoja wakati wa mkutano huo.
Wadau wa uchaguzi wakiwa ukumbini.
Wadau wa uchaguzi wakiwa ukumbini.
Wadau wa uchaguzi wakiwa ukumbini.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com