UJUMBE WA BENKI YA DUNIA WAKUTANA NA MTENDAJI MKUU-MAHAKAMA

Na Mary Gwera, Mahakama

Wataalamu kutoka Benki ya Dunia ‘World Bank’ wapo nchini kwa  lengo la kufanya tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama unaofadhiliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki  hiyo.

Lengo la Ujumbe huo kutembelea Mahakama ni kusaidia kukwamua vikwazo mbalimbali ili kuongeza kasi na ufanisi wa utekelezaji wa Mradi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha; Wataalam hao ambao watakuwepo nchini kwa muda wa siku saba (7), waliwasili nchini  Agosti 23, 2019 na tayari wametembelea baadhi ya Miradi ya ujenzi ya Majengo ya Mahakama Kuu Musoma-Mara, Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu pamoja na kukagua maendeleo ya ufanyaji kazi ya Mahakama inayotembea ‘Mobile Court’ mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kitengo cha Maboresho cha Mahakama (JDU), Ujumbe huo pia tayari umekutana na baadhi ya Ofisi/Kurugenzi mfano Kurugenzi ya Ugavi na Ununuzi na vilevile Wajumbe hao watapatiwa taarifa za hatua  za utekelezaji wa malengo mbalimbali yaliyowekwa kwa kila Idara/Kitengo.

Hali kadhalika, Agosti 27, 2019, Ujumbe huo ulipata wasaa wa kukutana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga na kufanya mazungumzo kuhusiana na utekelezaji wa Mradi huo.

Baada ya kukamilika kwa ratiba ya ugeni huo, watatoa maoni/mapendekezo ya maeneo ya kuyafanyia kazi zaidi ili kuboresha utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post