Na. Edward Kondela
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati ya upatikanaji wa vifaranga vingi vya samaki pamoja na chakula bora cha samaki sambamba na kuendelea kutoa elimu ya ufugaji ili wananchi waweze kufuga samaki kwa tija.
Akizungumza kwenye maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) kitaifa, katika viwanja vya Nyakabindi vilivyopo Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema serikali imelazimika kuweka mikakati hiyo kutokana na wananchi wengi kuwa na mwamko wa kufuga samaki kibiashara licha ya kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa vifaranga bora na chakula kwa bei nafuu.
“Kwa mfano mwaka jana uhitaji wa mbegu za samaki ulikuwa unafikia takriban samaki Milioni 40 lakini sisi tumeweza kuzalisha kama Milioni 18 kwa hiyo kuna mikakati ipo kuhakikisha vituo vya serikali pamoja na kuhamasisha vile vya watu binafsi kuzalisha vifaranga bora, changamoto nyingine ni chakula ambapo wapo wanaotengeneza hapa nchini lakini vinakuwa havijafikia ubora unaotakiwa na wengine wanaagiza kutoka nje ya nchi ambapo ni bei ghali, hivyo tunaweka mikakati ya uwepo wa chakula bora na bei nafuu pamoja kutoa elimu ya utengenezaji wa chakula hicho.” Amesema Dkt. Tamatamah
Amefafanua kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Maonesho ya Nanenane mwaka huu, sekta ya uvuvi imejikita zaidi katika kutoa elimu ya ufugaji bora wa samaki ili kuwavutia wananchi kuwekeza katika ufugaji samaki kibiashara.
Kuhusu ulaji wa samaki nchini Dkt. Tamatamah amesema kulingana na tafiti kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa sasa kila mtanzania anakula walau Kilogramu 8.2 za samaki kwa mwaka ilhali FAO inapendekeza mtu mmoja kula samaki kilogramu 20.3 kwa mwaka, hivyo serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiweka pia mikakati ya uwepo wa ongezeko la uzalishaji wa samaki hapa nchini lakini pia kuhakikisha samaki wachache wanaozalishwa wanamfikia mlaji wakiwa katika hali nzuri.
Katibu mkuu huyo anayeshughulika na sekta ya uvuvi amebainisha pia kupitia Maonesho ya 27 ya Nanenane kwa Mwaka 2019 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejikita zaidi katika utoaji wa elimu kwa wadau katika sekta za mifugo na uvuvi ili kutatua changamoto mbali zinazowakabili na kuweza kufuga kwa tija.
Mwisho.
Social Plugin