Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UTUPAJI HOLELA WA TAKA KUDHIBITWA

Na Lulu Mussa,Mwanza
Serikali imezitaka halmashauri zote nchini, kutenga maeneo maalumu mbali na makazi ya watu yatakayotumika kujenga madampo ya kisasa ili kuzingatia hifadhi ya mazingira.


Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa dampo la kisasa linalojengwa eneo la Buhongwa Jijini Mwanza.

Alisema ujenzi wa huo wa dampo la kisasa utasaidia juhudi za Serikali za kutotumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwa kuwa taka zitakazolishwa katika Jiji la Mwanza zitapelekwa dampo kwa wakati na kunusuru magonjwa ya mlipuko.

“Huwezi kutenganisha afya na mazingira, mradi huu ni mkubwa sana na kwa namna utakavyotekelezwa hatutaraji kuona taka mjini zinazagaa.Tunatarajia kuona taka zote zinakuja hapa,” alisema Sima.

“Natoa rai kwa halmashuri zingine ambazo zinatekeleza miradi ya kimkakati kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa madampo ya kisasa”.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba alisema dampo hilo lina ukubwa wa hekta 34 na linatarajia kukamilika desemba mwaka huu na kwa sasa ujenzi upo asilimia 78 ukigharimu Sh bilioni 16.6, ukienda sambamba na ujenzi wa barabara.

“Dampo hilo litakuwa na chemba sita za kuhifadhi taka na mabwawa ya kuhifadhi maji taka, barabara za kisasa zenye urefu wa kilomita 1.9, taa za nishati ya jua na maabara maalumu ya kupima maji taka” Kibamba alisema

Kukamilika kwa dampo hilo la kisasa litakuwa na uwezo wa kuteketeza taka mara baada ya kufikishwa kwenye eneo hilo na,litaongeza  mapato katika jiji hilo

Kwa mujibu wa Kibamba, tani 33 hadi 36 zinatarajia kupelekwa katika dampo hilo mara baada ya ujenzi kukamilika na linatarajia kudumu kwa zaidi ya miaka 15


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com