Utumbo
Mama mmoja mkazi wa Mbozi mwenye umri wa miaka 43 amefanyiwa upasuaji katika hospitali ya mkoa wa Songwe na kutolewa uvimbe mkubwa kwenye kizazi wenye uzito wa zaidi ya kilo 28.
Upasuaji huo umefanyika katika hospitali hiyo ambayo kila wiki hufanya upasuaji wa uvimbe kwa zaidi ya watu watatu.
Akiongea na East Africa Television daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama mkoa wa Songwe na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dr. Lukombodzo Lulandala, amesema katika upasuaji aliowahi kufanya hajawahi kukutana na uvimbe mkubwa wa kiasi hicho cha kilo 28.
Aidha Dr. Lukombodzo Lulandala amewataka wananchi mkoani Songwe, wasikimbilie kwa waganga wa kienyeji badala yake waonane na wataalaam wa afya.
Mgonjwa wa tatizo hilo,amewashukuru madaktari wa Mkoa wa Songwe kwa kuokoa maisha yake na kwamba sasa baada ya kufanyiwa upasuaji huo anaendelea vizuri huku akisema kwa zaidi ya miaka mitano amekuwa akihangaika na tatizo hilo.
''Naomba elimu itolewe kwani ndugu zangu walijua ni ujauzito, wahanga wengine wamekuwa wakihangaika sehemu mbalimbali bila kwenda hospitali kumbe wanaongeza tatizo'', amesema.