WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY MWALIMU , AZINDUA CHAMA CHA UREMBO NA VIPODOZI



Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, wazee, jinsia na watoto Ummy Mwalimu alipotembelea moja ya meza za vipodozi lipotemelea meza ya kutengeneza mawigi katika uzinduzi wa taasisi ya urembo na vipodozi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa ya ini, figo, moyo na saratani ambapo kwa mwaka 2015 wagonjwa wa kansa walikuwa 2416 hadi kufikia wagonjwa 7649 kwa mwaka 2018 na sababu mojawapo inayosababisha ni matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu vikali na amewashauri watengenezaji wa vipodozi kutengeneza mazingira bora ya biashara kwa kutengeneza bidhaa zinazokidhi viwango huku akiahidi ushirikiano katika suala zima la upatikanaji wa masoko.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, wazee, jinsia na watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa ongezeko la wagonjwa wa Kansa kutoka taasisi ya Kansa Ocean road imefikia wagonjwa 7649 mwaka 2018 ukilinganisha na wagonjwa 2416 mwaka 2015.Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa chama Cha urembo na vipodozi nchini (TCA), Waziri Ummy amesema kuwa amesukumwa sana mapinduzi yanayofanywa katika sekta ya urembo na vipodozi na amesukumwa zaidi kuhudhuria ufunguzi huo na akiwa mwanamke mwenye dhamana katika Wizara inayosimamia jinsia pia ameona hilo ni jambo jema la kuungwa mkono hasa sekta hiyo inahusisha afya pia.
Waziri Ummy amewapongeza waanzilishi wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao Shekha Nasser kufanikisha kuanzishwa kwa chama hicho na wao kama Wizara watahakikisha wanatengeneza mazingira bora ya biashara ili kuendeleza ujenzi wa viwanda pamoja na kuuza na kufanya biashara nje ya nchi.Vilevile amewashauri Mamlaka ya Elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) pamoja na baraza la taifa la elimu ya ufundi (NACTE) kuweka sehemu ya mafunzo katika sekta urembo katika mitaala ya elimu ili hata watu kutoka nje ya nchi waweze kuja kujifunza masuala ya urembo nchini na kuzidi kuipa thamani sekta hiyo, pia amewahakikishia wanachama hao kuwa serikali itaendelea kukuza sekta hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Vilevile ametoa rai watengenezaji na wauzaji wa vipodozi na urembo kufuata kanuni na taratibu pamoja na kuwashauri watanzania kukitumia chama hicho ili kuwe na sauti moja ya kuwasiliana na kufanya maamuzi kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Awali akizungumza katika hafla hiyo mwenyekiti wa chama hicho Shekha Nasser amesema kuwa tasnia hiyo inakua haraka duniani, barani Afrika na nchini Tanzania na kwa mwaka 2017 pekee ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 532 duniani huku ikitegemewa kufikia dola bilioni 863 kwa mwaka 2024 kwa ukuaji wa asilimia 7 kwa mwaka.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa chama hicho kumelenga kufanikisha malengo mbalimbali yakiwemo kuwaunganisha wadau wote wa sekta ya vipodozi na urembo pamoja na kukusanya maoni na kuyapeleka kwa serikali yakiwa na sauti moja na hiyo ni pamoja na kuendeleza viwanda vidogo, vya Kati na vikubwa na vinachangia sana katika kukuza ajira kwa vijana, kulipa kodi na mapato kwa serikali.
Baadhi ya wadau wa urembo wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, wazee, jinsia na watoto Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa taasisi ya urembo na vipodozi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Shekha amesema kuwa Tanzania inapata asilimia 3 pekee katika soko la dunia huku wanufaika wakubwa wakiwa ni nchi za Afrika kusini, Kenya na Nigeria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post