Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kumaliza changamoto ya miundombinu mibovu ya viwanja vya mpira nchini ili kuwezesha sekta ya michezo kufanya vizuri.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa mkoani Kagera katika mkutano na wadau wa sekta ya habari utamaduni sanaa na michezo uliofanyika katika ukumbi wa mkoa uliopo katika Bukoba manispaa.
Waziri Mwakyembe alisema anatambua sekta ya michezo kuwa sehemu muhimu na kwamba wanamichezo wanafanya kazi kubwa licha ya kukumbana na changamoto ya miundo mbinu mibovu ya viwanja vya michezo.
Alieleza kuwa tatizo la miundo mbinu mibovu ya viwanja limekuwa likipigiwa kelele mara kwa mara na wanamichezo licha ya kuonyesha juhudi kubwa katika michezo kwa kuendana na miundo mbinu hiyo mibovu.
"Changamoto hii itamalizika mwaka huu, tutalifanyia kazi jambo hili ili kupunguza kelele za viwanja vibovu vya soka nchini",alisema.
Licha ya changamoto hiyo waziri huyo aliwasihi wana michezo kutokata tamaa huku akiitaka Mikoa ya jirani na wana kagera kwa ujumla kujitokeza kwa wingi Septemba 4 wiki ijayo kuishangilia timu ya Taifa Stars inakutana kumenyana na timu ya Burundi, mchezo ambao ameuataja kuwa ni muhimu sana kwa Watanzania.
"Siri kubwa ya mafanikio ni mazoezi Vijana hakuna kusema kiatu kimebana tunakwenda kuifunga Burundi ninachowaomba wana Kagera, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikoa jirani twendeni Burundi tukaishangilie timu yetu", alisema.
Hata hivyo alisema Rekodi ya Tanzania ni nzuri kwani timu ya watoto wa kike chini ya miaka 17 ilikaribishwa Afrika Kusini kimichezo na kuwabamiza mabao 8-0 na kurudi Tanzania na kombe ikiwa ni mara ya tatu kuchukua ubingwa.
Social Plugin