Maelfu ya Waandamanaji katika Jimbo la Indonesia la Papua Magharibi jana wamechoma moto jengo la Bunge wakipinga kile wanachodai ni kukamatwa na kudhalilishwa kwa Wanafunzi.
Waandamanaji hao waliokuwa wakipinga vitendo hivyo vya udhalilishaji wanavyodai vinafanywa na vyombo vya dola dhidi ya Wanafunzi wa Papua, pia waliweka vizuizi barabarani.
Wanafunzi 43 katika maeneo ya Surabaya na Java Mashariki walikamatwa siku ya maadhimisho ya uhuru wa Indonesia baada ya bendera ya nchi hiyo kukutwa nje ya nyumba zao zikiwa zimeharibiwa.
Aidha, msemaji wa Polisi wa Java Mashariki, Frans Barung Mangera amesema kuwa wanafunzi hao waliachiwa huru baada ya kushikiliwa kwa saa kadhaa kutokana na kukosekana vithibitisho kuwa waliharibu bendera hizo.
Hata hivyo, waandamanaji walipatwa na hasira baada ya kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikiwaonyesha Polisi wakiwa na Wanajeshi wakiwaita Wanafunzi hao ‘Nyani’ na ‘Mbwa’
Gavana Msaidizi wa eneo hilo, Mohammad Lakotani amesema kuwa wakati mazungumzo yakiwa yanaendelea kati ya waandamanaji na Mamlaka, maandamano hayo yameharibu uchumi wa Papua Magharibi.
Social Plugin