Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Na Annastazia Paul - Malunde1 blog
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad na Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Suleiman Nchambi wamepongezwa kwa utendaji kazi wao mzuri hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wao wanaowaongoza.
Pongezi hizo kwa wabunge hao zimetolewa jana Agosti 22,2019 na Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Somagedi wilayani Kishapu ambapo amesema kwamba wabunge hao wanafanya kazi nzuri kwa maendeleo ya wananchi.
Akimzungumzia Mbunge Azza Hilal, Balozi Seif amesema kuwa "Kazi kubwa umeifanya maana mkoa huu ni mkubwa sana huna hata mfuko unaokusaidia, mwenzako huyu ana mfuko wa Jimbo unamsaidia saidia, nikuombe Mheshimiwa Azza jitahidini huko bungeni mpate mfuko maalum utakaowasaidia zaidi katika utendaji wenu, unafanya kazi nzuri sana".
Aidha amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kishapu,Mhe. Nchambi kwa kutekeleza vyema ilani ya CCM na kukamilisha miradi iliyoanzishwa na wananchi na ikiwemo kutoa mifuko 1200 ya saruji na mabati 400 kwa ajili ya kuikamilisha miradi ambayo inaendelea, iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi katika kata zote 25 za wilaya ya Kishapu.
Balozi Seif amewaomba wananchi wasirubuniwe na badala yake wawangalie vizuri wabunge hao kwani wanafaa na ni chachu katika maendeleo yao.
"Niwapongeze sana kwa kupata wabunge hawa wazuri na katika uchaguzi wa 2020 muwatizame vizuri",amesema Balozi Seif.
Katika hatua nyingine amewataka Wabunge wote kujijengea desturi ya kutembelea majimbo yao na kuzungumza na wananchi ili wazijue kero zao.
"Kaeni kwenye majimbo yenu ili muwe karibu na wapiga kura wenu, msikilize kero zao na mjue mahitaji yao". Amesema Balozi Seif.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji Mbunge wa viti maalum Mkoani Shinyanga,Mhe.Azza Hamad amesema kuwa jumla ya shilingi Milioni 130.8 zimetumika katika miradi ya sekta mbalimbali wilaya Kishapu ikiwemo afya, elimu na vikundi vya wanawake.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Suleiman Nchambi
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad.