Na Lulu Mussa, GEITA
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kata ya Mugusu Mkoani Geita wametakiwa kufuata taratibu za hifadhi ya mazingira ili kunusuru afya zao na kuchukua tahadhari ya kukabiliana na uwezekano wa milipuko ya magonjwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi kutembelea eneo la Mgusu, kuona uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
Akiwa katika eneo la Mugusu Naibu Waziri Sima amesema bado kuna tatizo la usafi wa mazingira katika maeneo wanayoyatumia kuchenjua dhahabu kwa kutumia zebaki, na kuna haja wachimbaji hao kukaa na halmashauri ya Geita Vijijini ili kuhakikisha wanakuwa na vyoo bora.
Akitoa kauli ya Serikali kuhusu mpango kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika shughuli za uchenjuaji, Sima amewataka wakazi wa Mgusu kuendelea na shughuli za uzalishaji wa dhahabu bila kuathiri sekta ya mazingira kwa kupunguza matumizi ya zebaki inayoharibu mazingira na afya za binadamu.
“Nimeona namna vijana wanavyojishughulisha kwa ajili ya kujipatia kipato, hili ni jambo jema kwenye Taifa letu, lakini nimetembea hadi chini kwenye ule mto wa Nyamasenge hakuna vyoo, watu wanatumia pori na mto kwa ajili ya haja ndogo na kubwa.
“Kwa mazingira yetu ni hatari sana, tunaweza kufanya kazi nzuri lakini ugonjwa utasitisha shughuli zetu. Nawasisitiza kuwa Usafi ni jambo la kwanza katika kufanya kazi, huwezi kuwa na nguvu isiyojali usafi,” alisema Sima.
Awali, Naibu Waziri Sima alitembelea chanzo cha maji cha maji cha Mto Mabubi na kujionea hali mbaya inayotishia kutoweka kwa chanzo hicho kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea kandokando ya eneo hilo.
“Chanzo cha maji cha mto Mabubi, hakitadumu na maji hayatakuwa salama kwa matumizi ya binadamu endapo kitaendelea kuingia kemikali ya zebaki nanyi wachimbaji kujisaidia katika eneo hilo” Sima alisisitiza.
Diwani wa Kata ya Mgusu Bw. Pastory Ruhusa amesema kuwa ataitisha mkutano wa wananchi mapema iwezekanavyo ili kuweka mikakati ya haraka kutokomeza hali hiyo ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira na kupunguza matumizi ya zebaki.
Naibu Waziri Sima yuko katika ziara ya kikazi Kanda ya Ziwa kukagua uzingatiaji na usimamizi wa Sheria ya Mazingira pamoja na uwaelimisha wananchi mpango wa Serikali wa kupunguza matumizi ya zebaki nchini.
Social Plugin