WAKULIMA WATAKIWA KUJIKITA KILIMO CHA UMWAGILIAJI NA KUCHANA DHANA YA KUTEGEMEA MVUA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Wakulima hapa nchini wametakiwa kuachana na kilimo cha kutegemea mvua na badala yake wametakiwa kujikita zaidi katika kilimo cha Umwagiliaji  ili kuwa na  Uhakika wa Mavuno na kuleta tija katika sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na   Mkuu wa  Mkoa wa Singida Dokta REHEMA NCHIMBI wakati akifunga kilele cha Maonesho ya  26  ya wakulima na Wafugaji Kanda ya kati  [NANENANE]  yaliyokuwa yakifanyika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Dokta Nchimbi ambaye alikuwa mgeni Rasmi katika Maonesho hayo amesema moja ya changamoto kubwa inayowakabili wakulima na wafugaji hapa nchini ni kilimo cha kutegemea mvua pekee hivyo wanatakiwa kuondokana na dhana hiyo na badala yake wabadilike na wajikite katika kilimo cha umwagiliaji huku pia akisisitiza suala la uvunaji wa maji ya mvua.

Aidha Dokta NCHIMBI amesema ni aibu kwa mikoa hiyo kulalalmika uwepo wa njaa ilhali ina ardhi ya kutosha inayofaa kwa kilimo na mifugo.

Dokta nchimbi amekumbusha suala la utunzaji wa mazingira na kuwashauri wakala wa misitu Tanzania kuacha kuendesha operesheni ya kuacha matumizi ya mkaa bali pia wawe na operesheni ya kusambaza mizinga ya nyuki ili kuwepo na shughuli mbadala.

Pia Amependekeza kuongezwa kwa tuzo mbili katika maonyesho ya mwaka ujao ambazo ni tuzo ya wavunaji bora wa maji ya mvua na wakulima bora wa malisho ya mifugo.

Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma dokta BINILITH MAHENGE amewataka wakulima waliopata utaalamu kupitia maonyesho hayo kuyatumia kwa vitendo.

Nae kaimu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge kilimo,mifugo na maji ambaye ni mbunge wa Singida Kaskazini Justine Monko amesema lengo la serikali ni kupunguza tozo mbalimbali zinazowakabili wakulima na wafugaji nchini na kama bunge linaunga mkono dhamira hiyo.

Maonesho hayo yamelenga kuwa shamba darasa kwa wakulima na wafugaji kujifunza yakiwa yameshirikisha kampuni zaidi ya 20,wajasiriamali zaidi ya mia Tatu,taasisi za serikali na binafsi zaidi ya 35 na  Kauli mbiu mwaka 2019 ni  Kilimo,Mifugo na Uvuvi kwa ukuaji wa uchumi wa nchi huku kitaifa yakifanyika mkoani Simiyu


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post