Na. Scola Malinga, WFM, Dar es Salaam
Serikali imejipanga upya kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa kupitia na kuboresha mwongozo wa ukopaji, utoaji wa dhamana na upokeaji misaada nchini.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Saalam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na mipango, Bw. Doto James,wakati wa ufunguzi wa warsha ya wakurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara mbalimbali iliyoangazia kujadili na kuweka mkakati wa mwongozo huo.
Bw. James alisema kuwa, chimbuko la Mwongozo huo ni changamoto ambazo Serikali imekuwa ikikabiliana nazo wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo hususan miradi inayotekelezwa kwa fedha za mikopo na misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo.
“Kama Wizara ya Fedha na Mipango, tumeshuhudia uwepo wa maandalizi duni ya miradi,na pia miradi kuchukua muda mrefu kuanza kutekelezwa na hivyo kuigharimu Serikali muda na fedha", alieleza Bw. James.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha, alieleza kuwa eneo lingine ambalo limekuwa na changamoto katika utekelezaji wa miradi ni misamaha ya kodi. Katika kulifanyia kazi jambo hilo, Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa taarifa na mapendekezo kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za masuala ya kodi ili miradi yote yenye changamoto za kodi itekelezwe ipasavyo kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi.
Bw. James, aliwasisitiza wakurugenzi hao kufanya majadiliano ya rasimu ya Mwongozo na kutoa mapendekezo ambayo yatatumika katika kukamilisha Mwongozo huo ili uje kusaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Aidha, Mwenyekiti wa Warsha hiyo ambaye ni Katibu Mkuu Msaafu, Bw. Peniel Lyimo, aliwasisitiza wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kusaidia usimamizi wa miradi ya serikali kwenye maeneo yao.
Bw. Lyimo aliwapongeza wajumbe wa mkutano kwa michango yao itakayowezesha kufanikisha kukamilika kwa mwongozo huo, ambapo utakapokamilia utasaidia katika kutekeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo na hivyo kuleta tija kwa wananchi.
Aidha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Amina Shaaban, alieleza kuwa, nchi ya Tanzania imeshuhudia kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani katika miaka ya karibuni, hususan kuanzia mwaka 2016. Pamoja na kuongezeka kwa mapato, bado nakisi ya bajeti imekuwa ikiongezeka kutokana na Serikali kujikita katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ukiwemo mradi wa Umeme wa Maporomoko ya mto Rufiji, Reli ya Kisasa kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ujenzi na ukarabati wa madaraja na miundombinu mbalimbali.
Alisema ili kuziba pengo la nakisi, Serikali imekuwa ikiingia katika michakato mbalimbali ya madeni, dhamana na misaada kwa kutumia sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Suraya 134.
Bi. Amina Shaaban alibainisha kuwa, changamoto iliyojitokeza miaka ya hivi karibuni, ni kupungua kwa mikopo yenye masharti nafuu (concessional loans), hivyo Serikali imelazimika kuingia katika mikopo ya kibiashara (commercial loans).
Aidha, mikopo hiyo huambatana na masharti magumu na hivyo huhitaji umakini mkubwa (responsible borrowing) ili kuepuka kuingiza Taifa katika mikopo isiyolipika.
Alisema kuwa pamoja na michango wajumbe wa warsha hiyo katika kupitia na kuboresha rasimu ya mwongozo huo, Serikali imejipanga kuutekeleza mara utakapokamilika.
Social Plugin