Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka amesema wanafunzi kidato cha nne waliopata daraja sifuri katika mtihani wa Mkoa wa Kujipima ‘Mock’ watawekwa katika kambi maalum ya kitaaluma na kufundishwa na walimu mahiri kwa lengo la kuwasaidia kuongeza ufaulu na kufikia daraja la nne na kuendelea, katika mtihani wa Taifa mwaka huu 2019.
Mtaka ameyasema hayo Agosti 22, 2019 katika kikao cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa Mock kwa wanafunzi wa kidato cha nne na matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita mwaka 2019, ambapo mkoa wa Simiyu umekuwa miongoni mwa mikoa kumi bora Kitaifa.
Mtaka amesema lengo la Mkoa ni kuona wanafunzi wote waanafanya vizuri na hakuna mwanafunzi wa kidato cha nne anapata daraja sifuri hivyo wanafunzi wote wenye daraja sifuri na wale walipata daraja la nne alama za mwisho watawekwa pamoja na kutafutiwa walimu mahiri ili wawasaidie kupanda kitaaluma na kupata ufaulu mzuri.
“ Tutaweka kambi ya wanafunzi wote waliopata sifuri kwenye mtihani wa ‘Mock’ lakini pia hata wale waliopata daraja daraja la nne alama zinazoashiria kuelekea kwenye sifuri, Siku sitini kabla ya mtihani wafundishwe masomo manne tu, Civics(Uraia), Kiswahili, Kiingereza na Historia ngalau wapate alama D ili wapate cheti; nia yetu kama mkoa ni kuona kila mwanafunzi anafanya vizuri" alisema
Katika hatua nyingine Mtaka amewahimiza wakuu wa shule kusimamia kwa karibu ufundishaji na kuhakikisha katika kipindi hiki kuelekea katika mitihani wa Taifa wa Kidato cha nne, kuongeza ufaulu kutoka nafasi ya tisa ya mwaka 2018 kwenda kwenye nafasi nzuri zaidi.
Afisa elimu wa mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amewataka wakuu wa shule na maafisa elimu kata na wilaya kuendelea kusimamia ufundishaji ili wanafunzi waweze kufanya vizuri na wale ambao shule zao hazikufanya vizuri waimarishe usimamizi ili kuongeza ufaulu.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Itilima amezungumzia kambi maalum za kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne waliopata sifuri kwenye mtihani wa Mock ambao wapo takribani 2000 kati ya wanafunzi zaidi ya 9000, kwamba zitakuwa msaada kwao na wanatarajia kuzifanya kwa ufanisi ili mkoa uwe kati ya mikoa tisa bora Kitaifa mwaka 2019(Single digit).
Mkuu wa mkoa ameahidi kutoa shilingi elfu 30 kwa mwalimu katika kila alama A itakayopatikana kwenye somo lake, shilingi milioni tano kwa shule itakayoingia kumi bora kitaifa, Milioni tano kwa Halmashauri itakayoingia kumi bora kitaifa, na milioni mbili kwa mwanafunzi atakayepata ufaulu daraja la kwanza pointi saba na kuwa katika kumi bora kitaifa na ikiwa hatakuwa miongoni mwa wanafunzi bora kitaifa atapewa shilingi milioni moja.
Mkutano wa tathimini ya matokeo ya kidato cha sita mkoani Simiyu unawakutanisha wakuu wa shule za sekondari,maafisa elimu wilaya ,wakurugenzi watendaji, wenyeviti wa halmashauri za wilaya na wenyeviti wa Kamati za Elimu za Halmashauri lengo likiwa ni kuangalia walipo na wanapoelekea katika maendeleo ya elimu mkoani Simiyu
MWISHO.