Na. Edward Kondela
Wawekezaji katika sekta ya ngozi wamewasili hapa nchini wakitokea nchini Misri kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara nchini humo kuanzia tarehe 8 hadi 10 Mwezi Julai Mwaka 2019 na kukutana na wadau wa ngozi nchini humo.
Akizungumza kufuatia ugeni huo uliowasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Felix Nandonde, amesema umetokana na ziara ya kikazi aliyofanya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa nchini Misri ambapo alipokuwa nchini humo alitembelea mji wa viwanda vya ngozi Roubiki na kuzungumza na wazalishaji wa bidhaa za ngozi nchini humo na kuwapa mwaliko wa kuja nchini Tanzania kuwekeza katika sekta ya ngozi kutokana na ubora wa bidhaa ya ngozi inayopatikana hapa nchini.
“Jambo moja kubwa tumeweza kuwathibitishia hawa wawekezaji katika sekta ya ngozi kutoka nchini Misri ni kwamba Tanzania ina bidhaa bora za ngozi na wenyewe wamejionea bidhaa bora za ngozi na ngozi yenyewe ambayo inapatikana nchini, wamekiri ni ngozi bora, tunaamini kwamba matunda ya ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa imeweza kufungua mlango wa sekta ya ngozi Tanzania.” Amesema Dkt. Nandonde
Kufuatia ugeni huo wa Bw. Mahmoud Sargy Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Sargy Tannery, Bw. Hisham Gazar Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Piel Color na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Kiwanda cha kuchakata ngozi Cairo for Investment and Development Mhandisi Yasser El Maghraby, Dkt. Nandonde amefafanua kuwa anaamini wawekezaji hao watapanga mipango ya muda mrefu na mfupi kuhakikisha wanashiriki kunyanyua sekta ya ngozi nchini Tanzania.
Kuhusu ubora wa ngozi Mkurugenzi huyo wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Felix Nandonde amesema wizara imejipanga kuzidi kutoa elimu kwa wachunaji wa ngozi ili wapate elimu sahihi ya uchunaji na kuwapatia mbinu bora ya uchunaji wa ngozi kwa kuwa ngozi machinjioni imekuwa ikipoteza ubora wake kwa asilimia 50 kutokana na uchunaji usiyo sahihi.
“Wizara kwa sasa imeanza kutoa mafunzo kwa wachunaji mfano Mkoa wa Morogoro kwa kuwa ngozi inapoteza ubora kutokana na kuharibiwa na visu wakati wa uchunaji hivyo kuwa na matundu na kupunguza ubora wa ngozi.” Ameongeza Dkt. Nandonde
Licha ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoa elimu ya ufugaji bora mkurugenzi huyo wa uzalishaji na masoko amewaasa wafugaji kufuga ng’ombe kwa njia bora, kuhakikisa wanawaogesha ili kujikinga dhidi ya magonjwa yanayoharibu ngozi pamoja na wafugaji kutowawekea alama mifugo yao sehemu zisizostahili ambazo zimekuwa zikisababisha kupoteza ubora wa ngozi.
Awali wawekezaji hao kutoka Misri mara baada ya kuwasili hapa nchini, waliambatana na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutembelea Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi WOISO kilichopo eneo la Salasala jijini Dar es Salaam wakiwa na lengo la kujionea namna ngozi inavyotumika kutengenezea bidhaa mbalimbali.
Wakiwa kiwandani hapo wameshuhudia idadi kubwa ya vijana walioajiriwa wakiwa katika majukumu yao ya kutengeneza bidhaa mbalimbali vikiwemo viatu, mikanda na mabegi ambapo walitaka kufahamu utendaji kazi wa kiwanda, teknolojia zinazotumika kiwandani hapo pamoja na soko la bidhaa hizo ili kuangalia maeneo ambayo wanaweza kushirikiana na wawekezaji waliopo hapa nchini katika sekta ya ngozi.
Aidha wakiwa jijini Dar es Salaam wawekezaji hao walipata fursa ya kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Ace Leather kilichopo mjini Morogoro Bw. Onorato Garavaglia, ambapo walitaka kufahamu pia namna kiwanda hicho kinavyopata ngozi na hatua inazopitia hadi kuchakata ngozi hiyo kabla ya kuipeleka sokoni.
Bw. Garavaglia aliwafahamisha umuhimu wa ujenzi wa kiwanda bora yakiwemo mazingira ambayo hayataathiri ubora wa ngozi na namna kiwanda chake kinavyozidi kujiimarisha kwa kufunga mitambo mipya ya kisasa zaidi ili kuchakata ngozi na kuiongezea thamani zaidi katika soko la kimataifa.
Baada ya mazungumzo hayo wawekezaji hao kutoka Misri Bw. Mahmoud Sargy Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Sargy Tannery, Bw. Hisham Gazar Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Piel Color na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Kiwanda cha kuchakata ngozi Cairo for Investment and Development Mhandisi Yasser El Maghraby ambao wameonesha nia ya kuwekeza nchini katika sekta ya ngozi walifika katika kiwanda hicho cha kuchakata ngozi Ace Leather mjini Morogoro na kujionea madaraja mbalimbali ya ngozi iliyochakatwa kiwandani hapo na kusema kuwa wamefurahishwa na ubora wa ngozi iliyopo hapa nchini.
Mwisho.