Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amewasili jijini Yokohama, Japan tarehe 26 Agosti kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD 7) utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.
Mkutano huu wa Saba utatanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Makatibu Wakuu na Mabalozi tarehe 25 na 26 Agosti 2019 ukifuatiwa na kikao cha Mawaziri tarehe 27 Agosti, 2019 na utahitimiswa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019. Kauli mbiu ya Mkutano huu ni “Kuendeleza Maendeleo ya Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi”.
Mkutano wa Saba pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.
Agenda za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa.
Kutokana na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, Mkutano wa TICAD 7 umeandaa ratiba maalum itakayozishirikisha taasisi binafsi na za umma kwenye majadiliano ya kibiashara yatakayofanyika tarehe 29 Agosti 2019. Lengo la majadiliano hayo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Serikali wamiliki wa Kampuni, wafanyabiashara na wawekezaji ili kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali ya kukuza baishara, uwekezaji na utalii kati ya Japan na Afrika.
Kadhalika wakati wa mkutano wa saba nchi zote za Afrika zimepatiwa nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na vivutio vya utalii za nchi husika. Tanzania kupitia Bodi ya Utalii (TTB) imejipanga kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini wakati wa mkutano huo.
Mkutano wa Saba wa TICAD utahitimishwa kwa Wakuu wa Nchi kupitisha Azimio la Yokohama na Mpango Kazi wa utekelezaji wa Azimio hilo. Serikali ya Japan ilianzisha jukwaa la majadiliano kati yake na nchi za Afrika mwaka 1993 kwa ajili ya kujadili maendeleo na nchi hizo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan.
26 Agosti 2019