Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini kukaa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kupitia kwa pamoja taratibu za usajili wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi nchini (CHAKUWATA) ambao hautambuliki katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilhali kinafanya kazi na wavuvi.
Waziri Mpina amesema hayo jana (07.08.2019) katika Maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi nchini (Nanenane) kwenye viwanja vya Nyakabindi katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea banda la Wizara ya Kilimo na kukuta uwepo wa chama hicho CHAKUWATA na kushangazwa kwa kuwa kinajishughulisha na wavuvi bila Wizara ya Mifugo na Uvuvi yenye dhamana na wavuvi kufahamu uwepo wake ambapo hakuridhishwa na sababu zilizotolewa na Naibu Mrajis Uhamasishaji kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Bw. Charles Malunde juu ya uhalali wa CHAKUWATA.
“Mpaka chama kinasajiliwa wizara haijui, lazima wizara ihusishwe katika hatua zote sasa kama katibu anayehusika na uvuvi hajui, mimi waziri sijui yaani hapa ndiyo tunashangaa kuna Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA). Sasa kwa sababu mmeshalifikisha hapa nia ya kuanzisha ushirika ni nzuri ibaki palepale lakini nyinyi (Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini) mkae muone namna bora kama kuna vitu havikufuatwa vikamilishwe kwa ukamilifu kwa sababu kuanzishwa huko bado hautuzuii kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza huko nyuma.” Amesema Waziri Mpina
Akitembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye maonesho hayo Waziri Mpina amesema ameridhishwa na umati wa watu unaofika katika banda hilo ili kupata elimu na kusema nia ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuwafikia wadau ili kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta za mifugo na uvuvi.
“Tunataka tuwahakikishie zile changamoto ambazo wametuwasilishia hapa tunaenda kuzifanyia kazi ili kuhakikisha tunapokutana mwaka mwingine wa Maonesho ya Nanenane zitakuwa zimesharekebishwa ili mwaka unaofuata wawe mashahidi kwa kushuhudia mageuzi makubwa ambayo yatakuwa yamefanyika.” Amefafanunua Waziri Mpina
Amefafanua kuwa baadhi ya changamoto kubwa ambazo amekutana nazo ni upungufu mkubwa wa chakula cha samaki na mifugo ambapo amesema anawahakikishia wadau katika sekta za mifugo na uvuvi katika kipindi kinachofuata Wizara ya Mifugo na Uvuvi itapanga mikakati madhubuti kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa.
Kuhusu masoko ya bidhaa mbalimbali zinazotokana na mifugo ambazo amezishuhudia kwenye Maonesho ya Nanenane Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina amesema wizara itahakikisha wadau wake wanatafutiwa soko la uhakika ili waweze kuuza mazao yao pamoja na bidhaa zinazotokana na mazao ya mifugo.
Akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara ambao wanashiriki katika Maonesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu, Waziri Mpina amesema ameridhishwa na namna wananchi wanavyohudumiwa kwa kupatiwa elimu na ufahamu juu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kesho (08.08.2019) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya Maonesho ya Nanenane kitaifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Nyakabindi vilivyopo katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
Mwisho
Social Plugin