NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema vituo vingi vya afya vinatibu wagonjwa wengi kienyeji bila kuwa na vipimo sahihi vya maabara.
Naibu Waziri huyo alisema inahitajika kuboresha huduma za maabara nchini kwa kuwa watu wanatibiwa kienyeji mno.
Alisema vituo hivyo vinatibu magonjwa yasiyosahihi kutokana na kukosekana kwa ufanisi katika huduma za uchunguzi wa maabara.
Dk.Ndugulile alitoa kauli hiyo juzi wakati akizindua Bodi ya nane ya Maabara Binafsi za Afya jijini Dodoma.
Alisema watu wamekuwa wakitibiwa kienyeji katika vituo vya kutolewa huduma kutokana na huduma za maabara kutofanya kikamilifu na vile ipasavyo.
Alibainisha kuwa maabara ni chombo muhimu sana katika sekta ya tiba inayotoa dira ya tiba sahihi kwa wagonjwa wanaohitaji huduma husika.
“Si hivyo tu, tafiti nyingi duniani zinahitaji maabara kuweza kupata ushindi wa kisayansi, hivyo bodi hii inajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa, maabara zinakuwa na ubora unaostahili kwa faida ya Watanzania na watu wengine kwa ujumla,”alisema.
Naibu Waziri huyo alisema inahitajika kuboresha huduma za maabara kwa kuwa watu wanatibiwa kienyeji sana.
“Nimekuwa nikiongeleza sana suala la kuwa na maambikizi ya mkojo -UTI, taifoid na homa, mgonjwa akienda hospitali anakaa dakika 15 anambiwa una UTI, anakaa dakika tano anaambiwa una typhoid, sijawahi kuona uchunguzi wa magonjwa haya wa dakika 15 nilivyofundishwa mimi uchunguzi unachukua kati ya saa 48 hadi 72 ,”alisema.
Alieleza kuwa hali ya sasa ya huduma za maabara zimekuwa ikitumika kufanya biashara na kuwa chanzo cha mapato kwa vituo vya kutolewa huduma huku akisema wagonjwa wengi wanatibiwa kwa magonjwa yasiyo sahihi.
“Zaidi ya asilimia 70 ya homa wanasema ni malaria wala sio malaria, watu wanakunywa dawa sana bila kuzingatia,”alionya Naibu Waziri.
Ndugulile alikemea tabia iliyoanza kuibuka kwenye maabara ya kuacha kutoa huduma za kimaabara na badala yake kutoa tiba na upasuaji.
“Maabara zimeanza kutumika kama sehemu za kutolewa matibabu, yule yule mtu wa maabara ndiyo daktari, wengine wameenda mbali zaidi maana maabara zimeanza kufanya upasuaji, hili halikubaliki,”alionya Naibu Waziri.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri huyo aliitaka bodi hiyo kwenda kutafakari na kuona namna ya kuja na mchakato wa mabadiliko ya sheria ambayo ni ya muda mrefu ili iende na wakati na pia kuongeza majukumu ya Bodi.
Alitaka majukumu yaongezwe badala ya kusimamia maabara binafsi pekee bali hata maabara za vituo vya hospitali za umma ambazo pia baadhi yake zimekuwa hazifanyi vizuri.
Akizungumzia kuhusu uanzishaji holela wa maabara, Dk.Ndugulile aliitaka bodi hiyo kukabiliana na hali hiyo kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
“Huko vichochoroni nikifanya ukaguzi hata hapa Dodoma naamini nitakuta maabara za uchochoroni ambazo hazina usajili zipo zinatoa huduma kwa wananchi lakini zipo maabara ambazo zinakwenda zaidi ya huduma za uchunguzi wa magonjwa,”alisema.
Aliitaka bodi hiyo kuja na kanzidata ya maabara na maduka yanayouza vifaa vya maabara na vitendanishi ili ifahamike yako magapi na yanafanya nini.
CHANZO - NIPASHE
Social Plugin