Na. Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali imeitaka Benki ya TPB na Benki nyingine nchini kuboresha mifumo ya huduma na bidhaa zao ili kuvutia Watumishi pamoja na Taasisi za Umma kutumia huduma zao.
Hayo yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Jacqueline Msongozi, aliyetaka kujua kwa nini Watumishi na shughuli zote za Serikali zisitumie huduma za kibenki kupitia Benki ya Serikali ya TPB.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ya uchumi huria, Serikali haina mamlaka ya kumlazimisha Mtumishi au Taasisi ya Umma kutumia huduma za benki yoyote ikiwemo Benki ya TPB.
“Kwa kuzingatia misingi ya nguvu ya soko, Benki ya TPB imefanikiwa kujitangaza na kuimarisha huduma na hivyo kuvutia baadhi ya Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma kutumia bidhaa zake”, alieleza Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji alisema huduma za Benki ya TPB zinazotumiwa na Taasisi za Serikali ni pamoja na akaunti ya muda maalumu, akaunti ya biashara, malipo kwa njia ya mtandao, kubadilisha fedha za kigeni, kukusanya mapato ya Serikali, kulipa mishahara ya Watumishi, mikopo kwa Watumishi, kulipa pensheni za Wastaafu pamoja na mikopo kwa Wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Serikali.
Alisema kuwa baada ya biashara huria ya Sekta ya Fedha na kupitishwa kwa sheria ya Benki ya Taasisi ya fedha kuanzia mwaka 1991, Wawekezaji mbalimbali walifungua benki binafsi nchini na hivyo matumizi ya huduma na bidhaa za benki kuanza kuamliwa na nguvu ya soko ikiwa ni pamoja na huduma na bidhaa za Benki za Serikali.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Madaba Mhe. Joseph Mhagama, kuhusu wafanyabiashara kushindwa kufanyabiashara kwa kukosa mitaji ili hali kuna Benki ya Serikali ya TPB, Dkt. Kijaji alisema kuwa Benki hiyo ina mfumo wa kuwasaidia Wajasiriamali kwa kuwapa mafunzo na mikopo iliyo na riba nafuu.
Aidha Benki ya TPB kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo Tanzania imetoa mikopo ya takribani Sh. bilioni 431 kwa Wakulima katika maeneo ambayo Benki ya Kilimo haina matawi, hivyo kusadifu dhima ya Serikali ya kuwafikia Wananchi wake katika kuwasaidia kukuza uchumi wao.
Social Plugin