Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDEGE YA AIR TANZANIA ILIYOKUWA INASHIKILIWA AFRIKA KUSINI YAACHIWA HURU

Mahakama Kuu ya jimbo la Gauteng imeamuru ndege ya Air Tanzania iliyokuwa ikishikiliwa nchini Afrika Kusini kuachiwa mara moja na mlalamikaji alipe gharama za kesi.

Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 ilizuiwa katika uwanja huo Agosti 23, 2019 kwa amri ya mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg ya Afrika Kusini baada ya Hermanus Steyn kufungua kesi katika mahakama hiyo akidai fidia ya dola 33 milioni.

Serikali ya Tanzania imesema kutokana na amri ya mahakama kushikiliwa ndege yake aina ya Airbus 200-300 nchini Afrika Kusini kutolewa bila mlalamikiwa kuwepo mahakamani, ilitumia jopo la wanasheria wa nchi mbili kushughulikia kesi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema toka kuzuiwa kwa ndege hiyo Jumamosi iliyopita Serikali ilimpeleka Afrika Kusini Naibu Waziri, Dk Damas Ndumbaro ili kushughulikia suala hilo.

Amesema ndege ilizuiliwa kwa amri ya mahakama kuu na kwamba ilikutana leo kutoa uamuzi ya maombi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ndege hiyo iachiwe baada ya kukamatwa kwa amri ya mahakama hiyohiyo ambayo ilisikilizwa kwa lugha ya kisheria ya kilatini bila mdaiwa kuwepo.

“Uamuzi huo umetenguliwa baada ya sisi kutoa maombi Jumanne na kuruhusu iachiwe kwa sababu ambazo Serikali na wanasheria wake walitoa na huku hii ya pili tunayo jaji ametoa uamuzi ndege hiyo iachiwe na ikabidhiwe kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Profesa Kabudi.

Amesema baada ya uamuzi huo wa mahakama sasa wanaendelea kufuatilia ana kwamba ndege hiyo inaweza sasa kuondoa nchini humo kurejea nchini.

“Tunawapongeza wanasheria wetu walioongozana na Naibu Waziri Dk Ndumbaro lakini pia timu ya wanasheria waliotoka kule nchini Afrika Kusini.”

Profesa Kabudi amesisitiza ndege hiyo ilishikiliwa kwa amri ya mahakama na si kwa maagizo ya Serikali ya Afrika Kusini.

Amesema ndege hiyo si ya shirika la ndege la Tanzania bali imekodishwa hivyo ni ndege za Serikali na kwamba shirika hilo linalipia fedha kila mwezi.

“Hizi ni ndege za walipa kodi ni za Serikali, zote zimenunuliwa kwa fedha za walipa kodi chini ya Rais John Magufuli.”

Aidha Profesa Kabudi amesema licha ya kuwepo kwa ndege hizo nane, Serikali inatarajia kuingiza ndege zingine kufikia mwishoni mwa mwaka huu, ikiwamo Dream liner moja, Airbus mbili na bombardier.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com