Na Leandra Gabriel, Globu ya Jamii.
Shule binafsi ya Precious Talent iliyopo Ngando, Nairobi nchini Kenya imefungwa hadi wiki ijayo ili kupisha uchunguzi wa vifo vya wanafunzi nane waliofariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa darasa hapo jana.
Kupitia televisheni ya Citizen nchini humo imeripotiwa kuwa mmiliki wa shule hiyo bado anahojiwa na jeshi la Polisi katika kituo cha cha kabete ambako baadhi ya wazazi pia wamefika kituoni hapo kwa ajili ya kuandikisha maelezo yao.
Mkuu wa polisi wa kituo cha polisi cha Kabete amesema kuwa uchunguzi umeanza kwa kuuliza maswali kwa mmiliki na kwa baadhi ya wazazi na baadaye kwa mamlaka zinazotoa vibali ya ujenzi, leseni na jengo na hatua zote za kusimamisha shule.
Vilevile amesema kuwa wanahitaji muda zaidi ili kuweza kufahamu chanzo hasa cha kuanguka kwa ukuta huo uliosababisha wanafunzi wanane kufariki dunia.
Imeelezwa kuwa mmoja ya wazazi waliofika kituoni hapo ameieleza Citizen Televisheni kwamba amempoteza mtoto wake wa miaka (13)aliyekuwa anasoma darasa la nane ambaye angefanya mtihani wa taifa mwaka huu.
Mzazi huyo ameeleza kuwa alitembelea shule hiyo siku ya Ijumaa na aliona sehemu ya darasa imedidimia na alipomuuliza mwalimu aliambiwa mahali hapo waliweka kuni na alihakikishiwa hakuna tatizo lolote.
Kufuatia janga hilo Serikali nchini humo itagharamia matibabu kwa majeruhi pamoja na mazishi kwa watoto waliopoteza maisha.
Social Plugin