GHARAMA ANAZOTAKIWA KULIPA MZUNGU ALIYEZUIA NDEGE AFRIKA KUSINI


Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi amefafanua agizo la Mahakama ya Guteng ya Afrika Kusini lililomtaka mkulima Herman Steyn kulipa gharama za kesi aliyofungua dhidi ya serikali ya Tanzania, hivyo kusababisha ndege ya ATCL kushikiliwa nchini, akisema gharama hizo ni pamoja na za malazi ya mawakili waliokwenda kuendesha kesi hiyo.

Gharama nyingine atakazotakiwa kulipa mkulima huyo ambazo pia zimo ndani ya kesi zilizoelezwa ni zinazohusu usafiri wa mawakili wa serikali kwenda nchini Afrika Kusini, usafiri wa ndani, gharama za mawasiliano yao kuhusu kesi hiyo, gharama za hoteli, chakula, vinywaji na huduma nyingine zinazoendana na malazi ambazo mawakili wa Tanzania walizitumia walipokwenda Afrika Kusini kwenye kesi hiyo.

Dk Kilangi alikuwa miongoni mwa wanasheria wabobezi waliokwenda nchini humo kwa ajili ya kesi hiyo. Alisema jana kuwa amri hiyo ya mahakama ina maanisha kuwa mzungu huyo hatahusika kulipia kitu kingine chochote wala fidia ya muda ndege iliposhikiliwa.

Agosti 24, mwaka huu ndege aina ya Airbus 220-300 ilishikiliwa Afrika Kusini kutokana na kesi iliyofunguliwa na Steyn, mlowezi aliyekuwa anamiliki ndege binafsi na mashamba mkoani Arusha, yaliyotaifishwa na serikali miaka ya 1980.

Alifungua madai ya kuzuia ndege hiyo akitaka kulipwa mamilioni ya fedha ikiwa ni malimbikizo ya fidia aliyokuwa akidai na kusababisha ndege hiyo kushikiliwa hadi ilipoachiwa baada ya siku 14.

Baada ya kesi hiyo kun- guruma kwa siku kadhaa, iliamuriwa ndege hiyo iachwe huru na mkulima huyo alipe gharama zote za kesi.

Kuhusu gharama halisi ambazo Mzungu huyo atatakiwa kulipa, Dk Kilangi alisema kwa sasa bado timu hiyo inaendelea na mchakato wa kubainisha ni kiasi gani kinachotakiwa kulipwa.

Alisema jamii itaelezwa gharama halisi baadaye. Alisema Mzungu huyo hatawajibika kulipia ghara- ma za hasara iliyotokana na muda wote ambao ndege hiyo ilikuwa haifanyi kazi, fidia kwa abiria, gharama za ndege, uegeshaji wa ndege kwenye Uwanja wa Oliver Thambo wala gharama za fidia ya kuharibiwa kwa haiba ya ndege hiyo.

Tangu kurejea nchini kwa ndege hiyo haijasafiri huku Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi akikanusha taarifa iliyo- sambaa kwenye mitandao ya kijamii jana kuwa ndege hiyo imeanza safari kwenda Afrika Kusini.

Credit:Habarileo


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post