Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HUDUMA ZA BENKI YA WANAWAKE KUTOLEWA NA BENKI YA TPB PLC

Na. Farida Ramadhan na Peter Haule, WFM, Dodoma

Serikali imesema kuwa kwa sasa hakuna Benki ya Wanawake Tanzania baada ya iliyokuwa Benki ya Wanawake kuunganishwa na Benki ya TPB Plc.

Hayo yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Faida Mohammed Bakar, aliyetaka kujua sababu zilizokwamisha uanzishwaji wa Benki ya Wanawake kwa upande wa Zanzibar.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, huduma za iliyokuwa Benki ya Wanawake Tanzania zinaendelea kutolewa na Benki ya TPB Plc ambapo imeanzisha dirisha maalum la wanawake katika matawi yake yote yakiwemo matawi ya Unguja na Pemba ili kukidhi mahitaji yao kote nchini.

“Nitoe wito kwa wanawake wa Tanzania watumie akaunti ya Tabasamu iliyopo katika Benki ya TPB Plc ili kunufaika na mikopo yenye riba nafuu bila kulazimika kuwa katika vikundi kama Benki zingine zinavyofanya”, alieleza Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Akaunti ya Tabasamu ilifunguliwa na Benki ya Posta kwa ajili ya Wanawake pekee kama Benki ya Wanawake ilivyokuwa ikifanya na pia inatoa mkopo kwa mwanamke mmoja mmoja kwa lengo la kumuwezesha  kufanya shughuli zake za kijasiriamali, kiuchumi na za kijamii kwa maslahi yake na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalum Mhe. Faida Mohammed Bakar, ameipongeza Serikali kwa majibu yake kwa kuunganisha Benki ya Posta na Benki ya Wanawake ili Wanawake waweze kuhudumiwa katika maeneo yote, ambapo awali huduma hizo zilikuwa zinapatikana katika maeneo machache kutokana na ufinyu wa matawi ya Benki ya Wanawake.

Mwisho.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com