Na Salvatory Ntandu
Zaidi ya wakazi 22,527 wanatarajia kunufaika na huduma ya maji safi na salama katika mji mdogo wa Isaka uliopo katika Halmashauri ya Msalala Mkoani Shinyanga, baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria ambao kwa sasa umeanza kutoa maji katika baadhi ya maeneo ya mji huo.
Hayo yamebainishwa leo na Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Isaka Rajabu Shabani wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa ,mradi huo umegharimu shilingi Bilioni 23 na utahudumia wakazi hao ambao watapata huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 98.
Amesema bado Mkandarasi anaendelea na ujenzi lakini baadhi ya maeneo maji yameanza kutoka katika magati mbalimbali ambapo kwa sasa wananchi wanachota maji hayo bure na ukikamilika na kukabidhiwa kwa serikali watatakiwa kulipia huduma hiyo pamoja na kuunganishishwa katika nyumba zao.
Naye diwani wa kata ya Isaka Jerald Mwenzia amesema Mji mdogo wa Isaka kwa sasa una mamlaka ambayo imesajiliwa kisheria na kwa hatua za awali wanaimba serikali kuwapunguzia wananchi gharama za kuunganishwa maji kama ilivyofanyika kwa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kahama(KUWASA)wakati waananza kutumia maji hayo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mwaluguru Flora Sagasaga amesema kupatikana kwa huduma ya maji katika kata ya isaka kumesaidia kuwatua ndoo akimamama ambao hapo awali walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 10 kutafuta huduma hiyo na kulazimika kutofanya kazi zingine za uzalishaji mali.
Amesema ndoa nyingi zilikuwa zikisambaratika kutokana na wanawake wengi kutoaminiwa na waume zao kutokana na kuchukua muda mrefu kufuata huduma ya maji katika visima au madimbwi ambayo sio salama kwa kutuhumiwa kujihusisha na uasherati pindi waendapo kuteka maji.
Betrice John na Limbu Masunga ni wakazi wa Isaka station wameishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi ya kuwapatia wananchi huduma ya maji ambayo ilikuwa ni tatizo kubwa ambalo kwa kipindi cha kiangazi maji hupanda bei hadi kufikia shilingi mia tano kwa ndoo moja.
Wamesema wakati mwingine walikuwa wanafuata maji katika wilaya jirani ya nzega mahali ambapo kuna visima visivyo kauka hali ambayo ilikuwa inawachukulia muda mrefu huku akinamama wajawazito wakishindwa kupata huduma hiyo kutokana na umbali wake kutoka katika mji huo wa Isaka.
Social Plugin