Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawilo akiongea na waandishi wa habari ambao hawapo pichani akiwa kwenye Gari lililokamatwa likisafirisha Kahawa kwenda Uganda bila kibali
Na Ashura Jumapili -Bukoba
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawilo,amemuagiza mkuu wa kituo cha polisi Bukoba ( OCD ) Babu Sanare,kuhakikisha anadhibiti magendo ya Kahawa yanayosafirishwa kupitia ziwa Victoria kwenda nje ya nchi kwa kuimarisha doria za majini.
Kinawilo ametoa agizo hilo leo baada ya gari lenye namba za usajili T.205 DHX Mitsubishi Fuso kukamatwa na gunia 115 za Kahawa jana majira ya saa nne usiku ilizokobolewa zilizokuwa zikisafirishwa bila kibali kwenda nchini Uganda.
Amesema Ziwa Victoria ni kichochoro kikubwa cha kusafirishia magendo ya Kahawa kwenda nchi jirani hivyo ni lazima kichochoro hicho kidhibitiwe kikamilifu.
"Ni ukweli kwamba magendo ya Kahawa yanapita ziwa Victoria kwenda nchi jirani.OCD ninakuagiza kuhakikisha unasimamia kwa ukaribu na kuongeza doria za majini ili kudhibiti usafirishaji wa magendo ya Kahawa.
Alisema miaka iliyopita Chama Kikuu cha Ushirika (KCU kilikuwa kinakusanya kilogram laki 7 za Kahawa kwa msimu na kwamba baada ya Serikali kuboresha mfumo wa uuzaji na ukusanyaji wa zao hilo msimu uliopita KCU walikusanya kilogramu milioni 13.
“Magendo ya kahawa hayakubaliki ikiuzwa kwa mfumo rasmi mkulima anapata mapato yake na serikalia pia inapata mapato”,alisema Kinawilo.
Alisema anatambua kazi nzuri inayofanywa na mkuu wa kituo cha polisi Bukoba ( OCD )na mpelelezi wa makosa ya jinai wilaya hiyo (OCCID ).
" Tunakesha usiku na mchana kamati ya ulinzi na usalama kuzuia na kudhibiti usafirishaji wa Kahawa za magendo kwenda nje ya nchi jambo hili halikubaliki hata kidogo" ,alisema mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha,aliwaagiza kuhakikisha kuwa wote waliohusika na utoroshaji wa Kahawa wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.
Mkuu wa kituo cha polisi Wilaya Bukoba ( OCD ) Babu Sanare alisema tukio la kukamatwa kwa kahawa hiyo lilitokea Septemba 24 mwaka huu Majira ya saa nne usiku.
Sanare,alisema askari waliokuwa doria walipata taarifa kuwa gari lilikuwa linasafirisha Kahawa bila kibali kwenda nchini Uganda kupitia Mwalo wa Bilolo Kemondo na kufanikiwa kukamata gari hilo maeneo ya Bulila Kata Kemondo iliyopo halmashauri ya Bukoba.
Alisema gari hilo lilikamatwa likiwa na gunia 115 ya Kahawa ilizokobolewa ambapo kila gunia lilikuwa na kilogramu 70 na watuhumiwa watatu na kudai kuwa dereva wa gari hilo alikimbia na kulitelekeza gari hilo baada ya kuona anataka kukamatwa na polisi.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Sadick Charles ,Jonizius Gerald na Lazaro Mdesa.
Alisema gari hilo baada ya kutelekezwa liliendeshwa na Askari namba G.9158 PC JOSEPH na kulifikisha kituo cha polisi Bukoba kwa hatua zaidi.
Alisema kuwa juhudi za kumtafuta dereva zinaendelea na watuhumiwa watatu wanashikiliwa kwa mahojiano.
Social Plugin