WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema kuwa idadi ya samaki waliopo nchini haitoshelezi kulingana na idadi ya Watanzania ambayo inazidi kuongezeka kila na kushindwa kila mtu kula wastani wa kilogram 14 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo kiasi cha samaki kinachozalishwa kwa mwaka ni tani 350,000 hadi 400,000 huku mahitaji ni tani 700,000 hali hiyo imesababisha kushuka kwa kiasi cha samaki kiliwacho kwa kila mtu kwa mwaka, kutoka kilo 14 mwanzoni mwa miaka ya 90 hadi kilo Nane (8) kwa mwaka 2019.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatamah wakati akifungua kikao kazi cha Wataalamu wa Sekta ya Uvuvi na wahariri wa Vyombo vya habari nchini ikiwa ni kutoa mwelekeo wa sekta ya uvuvi nchini.
Dk. Tamatamah amesema kiasi cha samaki wavuliwao kuanzia miaka ya 90 hadi sasa, kimebakia kuwa ni kati ya tani 350,000 na 400,000 kwa mwaka huku idadi ya watu ikiongezeka kutoka takribani watu milioni 25 hadi kufikia milioni 55.
“Hali hii inatishia ustawi wa taifa kwa vile samaki huchangia asilimia 30 ya protini itokanayo na wanyama na asilimia 1.7 ya pato la Taifa. Vilevile inachangia katika ajira na kipato ambapo zaidi ya watu milioni 4 wameajiriwa au kujiajiri katika shughuli zinazotegemea uwepo wa samaki,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa za utafiti zilizofanyika katika vipindi tofauti, kiasi cha samaki kilichopo katika maji yetu ni tani 2,803,000 ambapo mchanganuo wa kiasi unajumuisha tani 2,210,000 katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika Tani 295,000 na Ziwa Nyasa tani 168,000.
Alisema maji madogo (maziwa madogo na ya kati, mito na mabwawa) tani 30,000 na Maji ya Kitaifa ya Bahari ya Hindi tani 100,000.
Pia alisema katika mwaka 2018/19 kulikuwa na jumla ya wavuvi 202,053 nchini walioshiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uvuvi kwa kutumia vyombo vya uvuvi 58,930.
“Nguvu hii ya uvuvi iliwezesha kuvunwa kwa tani 448,468 zenye thamani ya Sh. Trilioni 2.11 sawa na ongezeko la asilimia 15.72 ya samaki (tani 387,543) zilivunwa mwaka 2017/18. Ongezeko hili limetokana na juhudi za Wizara katika kudhibiti uvuvi haramu nchini,” alisema.
Vilevile, alisema katika mwaka 2018/19 jumla ya tani 51,718.83 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 81,373 wenye thamani ya Sh.Bilioni 691.88 waliuzwa nje ya Nchi.
Aidha alisema katika kukabiliana na upungufu huo, serikali iliamua kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji, pamoja na kuanzisha idara ya ukuzaji viumbe maji kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza tasnia ili kuongeza uzalishaji wa samaki na viumbe maji wengine.
Pia Wizara kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo(FETA) kwa kushirikiana na NORGES VEL (Asasi isiyo ya kiserikali ya nchini Norway) na chama cha Wakuzaji Viumbe Maji Nchini(AAT) ilipata ufadhili wa Sh. Bilioni 4.6 kutoka Shirika la Misaada la nchini Norway(NORAD) kutekeleza mradi wa uzalishaji wa samaki aina ya Sato na kufundisha Stadi za Ufugaji na Biashara.
Aliongeza kuwa, Wizara inaendelea na juhudi za kufufua lililokuwa Shirika la Uvuvi Tanzania(TAFICO) ili kuimarisha uwekezaji katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari, na Bahari Kuu ambapo Menejimenti ya kusimamia ufufuaji wa TAFICO ilizinduliwa Julai, 2018.
Social Plugin