Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LUKUVI AZINDUA ULIPAJI KODI YA ARDHI KWA AIRTEL MONEY

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amezindua huduma ya ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa kutumia mtandao wa simu ya mkononi kupitia Airtel Money.

Uzinduzi wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya Airtel Money unarahisisha huduma hiyo ambapo wamiliki wa ardhi wataweza kufanya malipo kupitia mtandao huo wa simu bila kwenda ofisi za Ardhi.

Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 9 Septemba 2019 wakati wa kuzindua huduma hiyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema ubunifu wa serikali kufanya malipo ya Ankara za serikali kwa kutumia mfumo wa GePG umerahisisha malipo ya tozo mbalimbali za serikali ikiwemo kodi ya pango la ardhi.

Alisema mfumo huo wa malipo ya serikali umekuja na faida nyingi kama vile kuweka kumbukumbu vizuri, kulipa kwa muda, kupunguza upotevu wa mapato ya serikali, kuondoa mianya ya rushwa pamoja na kuongeza mapato ya serikali.

‘’Tunayo furaha kubwa kwa mara nyingine kutangaza kuwa kampuni ya simu ya Mkononi ya Airtel imerahisisha malipo ya kodi ya pango la ardhi kupitia Airtel Money. Hii ni huduma rahisi na itapunguza kero nyingi wakati wa kufanya malipo’’ alisema Lukuvi.

Aliitaka kampuni ya simu ya Airel kusaidia kuhimiza wananchi wanaotumia mtandao wa simu wa kampuni hiyo kulipia tozo mbalimbali za serikali ikiwemo kodi ya pango la ardhi kwa airtel money kwa kuwa inarahisisha kufanya malipo mahali popote.

Waziri Lukuvi amesema lengo la wizara yake kwa sasa ni kutaka kutumia makampuni ya simu kuwakumbusha wananchi kulipia kodi ya pango la ardhi kupitia jumbe za simu badala ya utaratibu uliopo sasa wa kwa kuwafuata wadaiwa.

‘’Sasa ofisi za ardhi za kulipia kodi ya pango la ardhi ziko viganjani mwenu mnaweza kulipia bila kwenda katika ofisi za ardhi’’alisema Lukuvi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Beatrice Singano alisema, kuunga mkono juhudi za serikali ni moja ya ajenda kubwa ya kampuni ya Airtel na kubainisha kuwa kampuni hiyo inaelewa umuhimu wa kukusanya kodi na kulipa malipo ya serikali kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo.

Kwa mujibu wa Singano, Airtel itaendelea kushirikiana na taasisi pamoja na mashirika mengine ya serikali kwa ajili ya kutimiza azma ya Serikali katika kukusanya mapato na kutoa wito kwa watanzania kuendelea kutumia huduma za kielektroniki kwa kuwa zina ubunifu mkubwa na kusisitiza kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na watanzania kwa asilimi 49 na matumizi ya mtandao  huo ni kutumia kilicho cha watanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com