Daraja la Nyabigufa linaloendelea kujengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Serikali ya Ubelgiji chini ya Mradi wa Sakirp – Enabel pamoja na wananchi lililopo katika mto Kaseke, Kijiji cha Nyabigufa Kata ya Mkongoro.
Daraja la Nyabigufa linaloendelea kujengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Serikali ya Ubelgiji chini ya Mradi wa Sakirp – Enabel pamoja na wananchi lililopo katika mto Kaseke, Kijiji cha Nyabigufa Kata ya Mkongoro.
Wananchi wa Kijiji cha Nyabigufa Kata ya Mkongoro katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wakiwa wanaendelea na ujenzi wa Daraja la Nyabigufa lililopo Mto Kaseke, Kata ya Mkongoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bi. Pendo E. Mangali akiwa na wataalam kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), wakati wa Ukaguzi wa daraja la Rubumba lililopo Kijiji cha Nyarubanda Kata ya Nyarubanda.
Daraja la mawe la Rubumba linalotarajiwa kukamilika hivi karibuni katika Kijiji cha Nyarubanda Kata ya Nyarubanda, kwa sasa wananchi wanatumia daraja la mbao kama linavoonekana katika picha.
Na Geofrey A.Kazaula na Bebi Kapenya - Kigoma
Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wanatarajia kunufaika na Ujenzi wa Madaraja ya mawe unaofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji chini ya mradi wa Kilimo endelevu katika Mkoa wa Kigoma (Sakirp – Enabel) na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kigoma Bi. Pendo E. Mangali ameeleza kuwa mradi huo uliibuliwa na wananchi baada ya kueleza changamoto wanayokutana nayo katika kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi majumbani na kwenye masoko.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa mradi huo wa Ujenzi wa madaraja ya mawe unalenga kutatua kero ya usafiri na usafirishaji wa mazao na kwamba wananchi walihamasishwa na wakakubali kujitokeza katika kusomba mawe na kushiriki kujenga madaraja hayo.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza sana wananchi wa Halmashauri ya Kigoma kwani wanafanya kazi sana, baada ya kugundua kuwa wanashindwa kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi sokoni kwa pamoja tuliamua kuanza ujenzi wa madaraja ya mawe”, amesema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa baada ya kukamilika kwa madaraja hayo kazi itakayokuwa imebaki ni Kufungua barabara za kuunganisha mashamba na hatimaye kuwezesha wananchi kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi na kukuza kipato chao.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mhandisi Pharles E. Ngeleja ameeleza kuwa Ujenzi wa madaraja kwa teknolojia ya kutumia mawe ni wa gharama nafuu na kwamba una washirikisha wananchi moja kwa moja kwa kukusanya vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao hususani mawe na wafadhili wanatoa vifaa vya viwandani visivyopatikana kwenye mazingira mfano simenti huku TARURA wakisimamia shughuli za ujenzi .
Akiongea kwa niaba ya wananchi wanaoshiriki katika ujenzi wa madaraja hayo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabigufa Ndg. Johnphace Kabora Tunzwe amesema kuwa changamoto ya usafiri ni kubwa hasa kipindi cha masika na hivyo tayari wameamua kujitolea kwa kukusanya mawe ili kujenga madaraja .
“Kwanza nawashukuru TARURA, Sakirp Enabel na Halmashauri ya Kigoma kwani mwanzo tulidhani kuwa kazi hii ni ngumu sana na haiwezekani lakini sasa kama mnavyoona tayari tumeanza kukamilisha ujenzi wa daraja” amesema Kiongozi huyo.
Aidha ameongeza kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa daraja, kazi itakayokuwa imebaki ni Kufungua barabara za kufika mashambani ili kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao na kwamba anaimani kuwa Serikali kupitia TARURA watafungua barabara .
Naye Meneja mshauri wa mradi huo chini ya Serikali ya Ubelgiji Ndg. Steven Hollevoet ameeleza kuwa Teknolojia ya ujenzi wa madaraja ya mawe ni ya muda mrefu hasa katika nchi za Ulaya na Asia na sasa wameileta Tanzania ili kuwafundisha wananchi kujenga madaraja kwa gharama nafuu kwasababu vifaa vinavyotakiwa kama mawe na mchanga vinapatikana kwa urahisi.
Hadi sasa madaraja sita yamekamilika na madaraja tisa yapo katika hatua mbalimbali huku lengo likiwa ni kukamilisha madaraja kumi na tano ifikapo mwezi Desemba, 2019.
Social Plugin