Mahakama ya Hakimu ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Vicnent Mashinji na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, waliokuwa wanaiomba mahakama hiyo kusafiri kwenda nje ya nchi kwa nyakati tofauti.
Mahakama hiyo imewataka washitakiwa hao bila kujali nyadhifa zao kuwepo mahakamani kama washitakiwa wengine. Washitakiwa hao sasa watatakiwa kujitetea kwa siku tano mfululizo kuanzia Oktoba 7 hadi 11, mwaka huu na mahakama inategemea hakutakuwepo na sababu nyingine zozote zitakazosababisha kesi hiyo isianze kusikilizwa kwa muda huo.
Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema, safari hizo ni mambo yao wenyewe na hayahusiani na ratiba ya mahakama. Amesema kuwa, iwapo mahakama itaruhusu maombi ya washtakiwa hao kusafiri, itakuwa imefungua mwanya kwa washtakiwa wengine hivyo haitaweza maombi ya wengine.
Hakimu ameongeza kuwa, kesi hiyo ni ya muda mrefu, inalalamikiwa sana, inatakiwa kusikilizwa na kufika mwisho, na Prof. Safari alisema wana mashahidi wengi hivyo kesi hii inahitaji kupangwa mara kwa mara kwa ajili ya kusikilizwa upande wa utetezi.
Mbali na Mashinji na Matiko, washitakiwa wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko la kutawanyika.
Social Plugin