Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewaomba Mawaziri wanaotaka kufanya ziara za miradi katika mkoa huo, kusitisha kwa muda ili kupisha utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa.
Amesema mwezi huu na Octoba watamalizia pia utekelezaji wa mikakati waliyopeana na kuanzia hapo mawaziri wataweza kufika na kuendelea na ziara zao za kikazi.
Makonda ameyasema hayo ni leo wakati akikagua mradi wa ujenzi machinjio ya kisasa ya Vingunguti ambao ujenzi wake umefika asilimia 25.
"Nawaomba mawaziri ambao wanataka kufanya ziara katika mkoa huu, tutekeleze miradi ambayo tumepewa maelekezo na Rais Magufuli alipofanya ziara na baada ya hapo waendelee kama walivyopanga," Makonda alisema.
Kuhusu ujenzi wa machinjio hayo alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kutekeleza mradi huo kwa haraka.
Makonda alimuagiza Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto, kukaa na baraza la madiwani kwa ajili ya kutenga fedha za kujenga barabara ya kuelekea katika machinjia hayo yenye urefu wa Kilometa moja.
"Baraza la madiwani likae litenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ya kuingia katika machinjio haya ya kisasa ili wafanyabishara wanaokuja wasikwame kwa sababu ya ubovu wa barabara," Makonda alisema.
Alisema pia kuwapo kwa machinjio hayo ni fursa kwa Manispa kujenga reli ya kuingia eneo hilo ili mizigo isafirishwe kwa treni.
Aidha, aliwataka kuangalia namna ya kuwalipa fidia wakazi wa maeneo hayo ili kuandaa eneo kwa ajili ya kupanua machinjio hayo kwa miaka ijayo.
Makonda alisema ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu na kuukabidhi kwa ajili ya kuanza shughuli za kuchinja ng'ombe.
Naye Mhandisi Elisante Ulomi, alisema wanamalizia kazi ya kushindilia kifusi kwa ajili ya kuanza kusuka nondo na kumwaga zege.
Alisema mwishoni mwa mwezi Novemba wataanza kupaua, wakati kazi za kufunga umeme na kumalizia kazi za ndani zikiendelea.
Naye Meya wa Ilala, Omary Kumbilamoto, alisema wanatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Makonda na kwamba lengo ni kuhakikisha mradi huo unakamilika Disemba na unakuwa kivutio.
Mbali na mradi huo, Makonda alitembelea mradi wa ujenzi wa soko la Kisutu na kuagiza mradi huo kukamilika mwezi Mei mwakani.
Social Plugin