Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba - Disemba 2019, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na wanyamapori, maliasili na utalii, nishati na maji, mamlaka za miji, afya pamoja na menejimenti za maafa.
Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma). Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake unaonesha kuwa:
a) Mvua za msimu wa Vuli, 2019
i. Maeneo yanayozunguka ukanda wa Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.
ii. Maeneo mengine yaliyosalia (Pwani ya Kaskazini pamoja na Nyanda za juu kaskazini Mashariki), mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.
iii. Maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2019 isipokuwa maeneo machache ya mkoa wa Kagera ambapo vipindi vya mvua za nje ya msimu zilizoanza toka mwezi Agosti 2019, vinatarajiwa kuendelea na hivyo kuungana na kuanza kwa msimu wa mvua za Vuli.
b) Athari zinazotarajiwa
i. Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua nyingi matukio ya magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza, hali kadhalika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani magonjwa ya mlipuko pia yanaweza kujitokeza kutokana na uhaba wa maji safi na salama.
ii. Upungufu wa malisho hususani katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani unaweza kujitokeza. Hali hiyo inaweza kusababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
iii. Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na chini ya wastani.
(I) MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KIPINDI CHA OKTOBA – DISEMBA, 2019
Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi cha Oktoba – Disemba, 2019 (kipengele II cha taarifa hii), mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na Pwani ya kaskazini. Aidha, maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (Kibondo) yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
1. Mvua za msimu wa Vuli
Msimu wa mvua za Oktoba – Disemba (Vuli) ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki, pwani ya Kaskazini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Katika msimu wa Vuli, 2019 maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani. Aidha, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
1.1 Kanda ya Ziwa Viktoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga):
Maeneo machache ya mkoa wa Kagera mvua za nje ya msimu zinaendelea toka mwezi Agosti na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine ya ziwa Viktoria hadi kufikia wiki ya pili ya mwezi Oktoba, Hivyo kuungana na msimu wa mvua za Vuli.
Mvua hizo zinatarajiwa kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba. Kiwango cha mvua kinachotarajiwa katika msimu huu ni mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda huo. Msimu wa mvua za Vuli katika maeneo haya unatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2020.
1.2 Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu. Vipindi virefu vya ukavu na mvua chache pia vinatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini. Hata hivyo, mvua zinatarajiwa kunyesha katika kiwango cha wastani kuanzia wiki ya pili ya mwezi Novemba. Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba.
1.3 Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua katika maeneo ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba 2019.
(II) MIFUMO YA HALI YA HEWA
Hali ya joto la bahari la juu ya wastani katika maeneo ya kati mwa bahari ya Hindi, kusini-magharibi pamoja na kaskazini magharibi (pwani ya Somalia) mwa Bahari ya Hindi inatarajiwa kuendelea katika kipindi chote cha Oktoba-Disemba 2019.
Hali hiyo inatarajiwa kusababisha mtawanyiko wa upepo kutoka katika pwani ya Tanzania kuelekea katikati ya Bahari ya Hindi. Hivyo, kusababisha vipindi vya upungufu wa mvua katika maeneo ya pwani ya kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki.
Aidha, joto la juu ya wastani katika Bahari ya Hindi linatarajiwa kuongeza uwezekano wa matukio ya vimbunga katika maeneo ya kusini-magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Kwa upande mwingine, joto la chini ya wastani linatarajiwa kuendelea kusini-mashariki mwa Bahari ya Atlantiki (karibu na pwani ya Angola) na hivyo inatarajiwa kuwepo kwa msukumo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo, na kusababisha mvua katika maeneo ya magharibi mwa nchi.
Uwepo wa hali ya joto la wastani katika eneo la kati la kitropiki la Bahari ya Pasifiki unatarajiwa kuwa na mchango hafifu katika mwenendo wa mifumo ya mvua nchini kwa kipindi cha Oktoba-Disemba, 2019.
(III) ATHARI NA USHAURI
Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, upungufu wa unyevunyevu ardhini unatarajiwa kujitokeza. Upungufu wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo pia unatarajiwa hivyo kusababisha uwezekano wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Wafugaji wanahamasishwa na kushauriwa kuvuna mifugo yao ikiwa bado katika hali nzuri. Wafugaji pia wanashauriwa kutunza mifugo yao kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa ugani katika maeneo yao.
Sekta ya uvuvi, katika maeneo hayo, inaweza kuathiriwa kutokana na upungufu wa maji katika mabwawa ya samaki na hivyo wafugaji wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya ufugaji wa samaki na kuzingatia matumizi sahihi ya maji.
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, shughuli za kawaida za kilimo zinatarajiwa. Aidha, malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo na wanyamapori vinatarajiwa.
Nishati, Maji na Madini
Upatikanaji wa maji unatarajiwa kuimarika, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Kina cha maji katika mabwawa na mito kinatarajiwa kuongezeka.
Hata hivyo, athari katika miundombinu ya rasilimali maji inaweza kujitokeza. Shughuli za uchimbaji madini katika migodi midogomidogo zifanyike kwa kuzingatia tahadhari zinazotolewa kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi. Aidha, maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini, ambapo mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa, kina cha maji katika mabwawa kinatarajiwa kupungua, hivyo matumizi sahihi ya maji kwa ajili ya umwagiliaji, majumbani pamoja na kuendesha mitambo ya umeme yanashauriwa.
Aidha, matumizi ya nishati mbadala za umeme yanashauriwa ili kuzuia upungufu unaoweza kujitokeza.
Mamlaka za Miji
Huduma za maji safi na maji taka zinaweza kuathirika, hususan katika vipindi vya mvua kubwa, hivyo, Mamlaka za miji pamoja na wananchi wanashauriwa kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji zinafanyakazi katika kiwango cha kutosha ili kuepusha maji kutuama na kupelekea mafuriko na athari nyingine.
Sekta ya Afya
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua nyingi matukio ya magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza. Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza mara kwa mara, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.
Aidha, matumizi ya maji yasiyo salama katika jamii yanaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko yanayohusiana na maji. Hivyo, ushauri unatolewa kwa mamlaka husika na jamii kuchukua hatua stahiki kupunguza athari za kiafya zinazoweza kujitokeza.
Menejimenti za Maafa
Menejimenti za maafa zinashauriwa kuandaa mikakati ya kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za Vuli 2019. Kuandaa mbinu za kukabiliana na mafuriko na vipindi vya ukavu, kama vile kuimarisha na kutenga rasilimali tayari kwa ajili ya kukabiliana na athari zinazoweza kijitokeza. Aidha, inashauriwa kuimarisha programu na njia za mawasiliano katika ngazi mbalimbali.
Vyombo vya habari
Ushauri unatolewa kwa vyombo vya habari kufuatilia mara kwa mara na kusambaza taarifa sahihi za mwenendo wa hali ya hewa na mirejeo inayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Wanahabari wanashauriwa kutafuta na kutumia maelezo ya wataalam wa sekta husika katika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kwa jamii.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika.