Tanzania ni miongoni mwa baadhi ya Nchi zinazotarajiwa kunufaika na kiasi cha dola za Kimarekani milioni 120 zilizotengwa na Serikali ya Marekani kwa ajili ya utafiti wa kupambana na ugonjwa wa seli mundi (sickle cell).
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya wa Marekani Admiral Brett Giroir wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi jijini New York Nchini Marekani.
Admiral Brett ameutaja mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi kama mwanzo mpya wa ushirikiano baina ya Tanzania na Marekani na kuongeza kuwa Nchi yake ina nyenzo zote ikiwemo teknolojia ya kupambana na maradhi ya seli mundu ili kuboresha Maisha ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa katika siku za hivi karibuni Tanzania imekuwa ikipiga hatua chanya katika kuimarisha masuala mbalimbali ya afya za wananchi wake na kwamba ni azma ya Marekani kuona kuwa ugonjwa wa seli mundo unapata tiba.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema utafiti na hatimae tiba ya maradhi hayo ya seli mundu kwa kiasi kikubwa itainufaisha Tanzania kutokana na kushika nafasi ya tatu katika Bara la Afrika na ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa seli Mundu.
Ameongeza kuwa Tanzania na Marekani zitashirikiana katika kufundisha na kujengeana uwezo wa namna ya kupambana na maradhi ya seli mundu lakini pia kutafuta fedha zitakazowezesha upatikanaji wa dawa ya seli mundu kutokana na ukweli kuwa dawa za ugonjwa huo kwa Tanzania ni miongoni mwa dawa muhimu yaani essential drugs ili iweze kuwafikia wananchi wengi na kwa bei nafuu.
Amezitaja Nchi zilizo na idadi ya watoto wengi wanaozaliwa na ugonjwa wa seli mundu ambapo kwa Afrika Tanzania ni ya tatu baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Nigeria nay a nne duniani baada ya India.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
New York,Marekani
Social Plugin