Rais Donald Trump amesema Marekani iko tayari kujibu mashambulizi yaliyofanywa katika miundo mbinu ya mafuta ya Saudi Arabia, mashambulizi ambayo Marekani imeoinyoshea kidole cha lawama Iran.
Mashambulizi hayo yamesababisha kuongezeka kwa kiwango kikubwa kwa bei ya mafuta duniani.
Hii ni mara ya kwanza kwa rais huyo wa Marekani kudokeza kuwa Marekani huenda ikajibu kijeshi mashambulizi hayo yaliyofanywa na ndege isiyo na rubani ambayo yamepunguza uzalishaji mafuta wa Saudi Arabia kwa nusu na kuifanya nchi hiyo ya kifalme pamoja na Marekani kusema kuwa huenda wakaamrisha kutumika kwa hifadhi zao za mafuta iwapo kutakuwa na upungufu.
Katika ujumbe alioutoa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Trump ameandika na hapa nanukuu "Usambazaji mafuta wa Saudi Arabia umeshambuliwa. Kuna sababu ya kuamini kwamba tunamjua mhusika, tuko tayari kabisa kulipiza kwa kutegemea na thibitisho lakini tunasubiri Saudi Arabia iseme inayeamini ndiye mhusika wa shambulizi hili," mwisho wa kunukuu.
Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wamedai kuhusika na mashambulizi hayo katika visima viwili vya mafuta vinavyomilikiwa na kampuni kubwa ya mafuta ya Saudi Arabia, Aramco.
Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ameinyoshea kidole cha lawama Iran akisema hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa mashambulizi hayo yalitokea Yemen.
Iran imeghadhabishwa na kauli hiyo ya Pompeo na msemaji wa wizara ya mambo ya nje Abbas Mousavi amesema madai hayo yasiyo na mwelekeo hayana maana.
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman amesema nchi hiyo iko tayari kujibu mashambulizi hayo aliyoyataja kuwa ya kigaidi.
-DW
Social Plugin