MCHUNGAJI ANAYEDAIWA KUTENGENEZA 'MCHAWI FEKI' IRINGA APINGANA NA POLISI



Kushoto ni RPC Iringa, Juma Bwire na kulia ni mama anayedaiwa kuwa Mchawi, Magreth Simon.

Mchungaji Jeremiah Charles mkazi wa Ilula mkoani Iringa, aliyezua gumzo hivi karibuni mara baada ya mwanamke aliyedaiwa kufanya mambo ya kishirikina kuganda juu ya nyumba yake, ameeleza kushangazwa na taarifa zinazoeleza kuwa mchawi huyo alilipwa pesa ili afanye kimbwanga hicho.

Hayo ameyabainisha leo Septemba 4, 2019 wakati akizungumza na EATV & EA Radio Digital na kusema kuwa, anahisi kuna mchezo umefanyika kwa jambo la ukweli kugeuzwa kuwa ni la uongo, kwani mtuhumiwa huyo amekaa muda mrefu polisi bila kufikishwa mahakamani na yeye anachoamini anafanyakazi ya Mungu na wala hahusiki na kutoa hongo yoyote kwa mwanamke huyo.

''Wale polisi kazi yao ni polisi, mimi ni mtumishi na mtumishi anafanya kazi ya kiroho na wao wanafanyakazi ya Serikali, haya mambo ya kiroho watayajua upana wake kivipi, mambo ya imani wanayajua watumishi, mimi ndo najua kwamba, imani yangu nilivyoomba Mungu ndiye aliyejibu, kwahiyo wao kama wamefanya uchunguzi ni wa kibinadamu, mimi ninachokijua katika ulimwengu wa kiroho kuna vita kati ya Shetani na Mungu, na nguvu ya Mungu siku zote itabaki kuwa juu.'' amesema Mchungaji Jeremiah.

Tukio hilo la mwanamke kukutwa juu ya paa akiwa amevalia mavazi meusi na ungo, lilitokea mwishoni mwa mwezi wa Agosti, ambapo Jeshi la Polisi Iringa lilimshikilia mwanamke huyo kwa ajili ya mahojiano na siku ya jana ya Septemba 3,2019 ilitoa taaarifa iliyoeleza udanganyifu uliofanywa na mwanamke huyo, ikiwemo ukweli wa tukio lenyewe pamoja na majina na mkoa aliotoka.
Chanzo-EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post