MILA POTOFU CHANZO CHA KAYA ZAIDI ELFU KUTOJENGA VYOO SHINYANGA

NA SALVATORY NTANDU

Kaya elfu 7,195  katika  mkoa Shinyanga zimebainika kutokuwa na vyoo  na kuendelea kujisaidia vichanani hali ambayo inaweza kusababisha kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kama vile homa za matumbo na hata kipindupindu.

Hayo yamebainishwa  jana na Afisa Mazingira wa mkoa wa Shinyanga Neema Simba, katika ufunguzi wa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora ijulikanayo kama “usichukulie poa nyumba ni choo” ambayo imeanza rasmi katika mkoa huo.

Amesema kuwa mwaka 2012 hali ya vyoo bora ilikuwa asilimia 17 na baada ya utekelezaji kampeni ya ujenzi wa vyoo bora imeboreka na kufikia  asilimia 50.6 ambapo malengo ya mkoa ni hadi kufikia desema mwaka huu kila kaya iwe na choo bora.

Amefafanua kuwa Halmashauri ya Mji wa kahama ina asilimia 75 vyoo bora ni asilimia 0.2 hazina vyoo, Halmashauri ya Kishapu asilimia 71 vyoo bora asilimia 2 hazina vyoo,Halmashauri ya Msalala asilimia 57.3 vyoo bora asilimia 4.4 hazina vyoo.

Halmashauri ya Shinyanga vijijini asilimia 19.7 vyoo bora asilimia3.9 hazina vyoo.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga asilimia 64 vyoo bora asilimia 0.9 hazina vyoo,Halmashauri ya Ushetu asilimia 20.9 vyoo bora asilimia 5.1

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amewaagiza wakurugenzi wote wa Mamlaka za serikali za mitaa katika mkoa huo kutoa elimu kwa wananchi wanaoendelea na mila potofu ikiwemo ya kutochangia choo kimoja na wakwe hali ambayo inasababisha wananchi kuendelea kujisaidia vichakani na kuchafua mazingira.

Nae Elizabeth Malingumu Afisa mwelimishaji kutoka wizara ya afya na maendeleo ya jamii wazee jinsia na watoto amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 kila nyumba hapa nchini iwe na afya bora na kuwataka wananchi wa mkoa wa shinyanga kuhakikisha wanajenga vyoo bora.

Kampeni ya nyumba ni choo itadumu kwa siku 22 katika mkoa wa shinyanga ambayo inaongozwa na balozi mkuu Msanii Mrisho Mpoto ambapo watazunguka katika halmashauri sita za mkoa huo ambayo inalenga kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post